Waziri wa Ulinzi wa Iran: Tumejiweka tayari kujibu chokochoko zozote za Israel
(last modified Thu, 10 Jul 2025 13:44:30 GMT )
Jul 10, 2025 13:44 UTC
  • Waziri wa Ulinzi wa Iran: Tumejiweka tayari kujibu chokochoko zozote za Israel

Waziri wa Ulinzi wa Iran Brigedia Jenerali Aziz Nasirzadeh amesema Vikosi vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu vimejipanga kikamilifu kutoa jibu kali kwa chokochoko zozote zitakazofanywa na utawala mtendaji jinai wa kizayuni wa Israel na waungaji mkono wake wa Magharibi.

Nasirzadeh ameyasema hayo katika mazungumzo aliyofanya kwa njia simu kwa nyakati tofauti na mawaziri wenzake wa ulinzi wa Venezuela na Armenia, Vladimir Padrino López na Suren Papikyan.

"Shambulizi kali la Vikosi vya Ulinzi vya Iran dhidi ya uchokozi wa utawala wa Kizayuni liliufanya utawala huo utoe ombi la kusitishwa kwa mapigano”.

Aidha, ameshukuru misimamo thabiti ya wananchi na viongozi wa Venezuela na Armenia wa kulaani vitendo vya kichokozi vilivyofanya mwezi uliopita na utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Waziri wa Ulinzi wa Iran amesema utawala ghasibu wa Israel ulifanya vitendo vyake vya uchokozi dhidi ya taifa hili wakati wa mazungumzo kati ya Tehran na Washington pamoja na mataifa matatu ya Ulaya ya Uingereza, Ufaransa na Ujerumani (E3).

Amebainisha kuwa, hatua hiyo ilionyesha kwa mara nyingine kuwa Marekani na pande zingine za Magharibi haziwezi kuaminika.

Katika mazungumzo hayo ya simu, Waziri wa Ulinzi wa Venezuela, Vladimir Padrino Lopez amesema, utawala wa Israel na waungaji mkono wake hawataweza kusababisha madhara kwa utamaduni usioyumba wa Muqawama wa taifa la Iran.

López ameongeza kuwa nchi za Amerika ya Kusini zitasimama upande wa Iran katika vita vyake dhidi ya mabeberu wa kimataifa.

 

Naye Waziri wa Ulinzi wa Armenia Suren Papikyan amelaani mauaji ya kigaidi yaliyofanywa na utawala haramu wa Israel dhidi ya watu wasio na hatia wa Iran pamoja na makamanda wa kijeshi.../