Kadhaa wauawa katika shambulio la al-Shabaab, Garissa Kenya
Watu wawili wameuawa huku wengine kadhaa wakijeruhiwa katika shambulio linaloshukiwa kuwa la magaidi wa al-Shabaab katika Kaunti ya Garissa, kaskazini mashariki mwa Kenya.
Wahanga wa hujuma hiyo ya jana Jumatatu waliotambuliwa kama Mohamed Shabel Bashir na Abdikadir Muhumed Salat, walikuwa wakisafiri kwa gari aina ya Probox kuelekea mji wa Bodhai, wakati mripuko mbaya ulipotokea.
Naibu Kamishna wa Kaunti ya Bodhai, Dubat Mohamed alithibitisha kisa hicho, akisema kilipuzi cha kuelekezwa tokea mbali cha IED kinaaminika kutegwa na wanamgambo wa al-Shabaab ambao hulenga maafisa usalama wanaoshika doria na hutumia njia hiyo mara kwa mara.
Haya yanajiri wiki chache baada ya wafanyakazi watano wa machimbo kuuawa huku wengine kadhaa wakijeruhiwa wakati gari lao liliposhambuliwa na watu wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wa kundi la kigadi la al-Shabaab karibu na kijiji cha Bur Abor katika Kaunti ya Mandera, kaskazini mashariki mwa Kenya.
Magaidi wa al-Shabaab wamekuwa wakiendesha uasi dhidi ya serikali ya Somalia tangu mwaka 2007, wakitaka kutwaa mamlaka na kuanzisha utawala kwa kuzingatia tafsiri yao kali ya sheria za Kiislamu. Kundi hilo la kigaidi lenya mfungamano na mtandao wa al-Qaeda, mara nyingi huvuka mpaka na kuingia nchini Kenya kufanya mashambulizi.
Genge hilo linadai kuwa linafanya hujuma hizo dhidi ya maafisa usalama na raia wa Kenya kwa kuwa nchi hiyo ndio mchangiaji mkubwa wa wanajeshi katika kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia.