Iran yamuonya mkuu wa IAEA: Vitisho vilivyofeli havitaleta isipokuwa kusindwa kwingine
-
Abbas Araghchi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amemuonya mkuu wa shirika la nyuklia la Umoja wa Mataifa, Rafael Grossi, dhidi ya kutoa "vitisho vilivyoshindwa" dhidi ya Tehran, akisema matamshi kama hayo hayataleta "isipokuwa kushindwa kwingine."
Matamshi ya Araghchi, jana Alhamisi, yametolewa baada ya Grossi kuliambia gazeti la kila siku la Uswisi, Le Temps, kwamba licha ya mashambulizi ya Marekani mwezi Juni yaliyopiga vituo muhimu vya nyuklia vya Iran, utaalamu wa kiufundi wa nchi hiyo bado uko palepale na haujaguswa.
"Sijui kama ametoa kauli hiyo kutokana na wasiwasi au kama tishio," amesema Araghchi na kuongeza kuwa: "Lakini wale wanaotoa vitisho hivyo lazima watambue kwamba kurudia tukio lililoshindwa hakutakuwa na matokeo yoyote ila kushindwa kwingine."
Akizungumzia athari za mashambulizi ya Marekani kwenye vituo vya nyuklia vya Iran, Rafael Grossi amesema akiba ya urani iliyorutubishwa ya Iran - takriban kilo 400 iliyorutubishwa hadi 60% - imebaki chini ya kiwango cha silaha ya nyuklia na ndani ya viwango vya matumizi ya amani.
Grossi amesisitiza kwamba Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) unataka kuanza tena ukaguzi kamili nchini Iran lakini ufuatiliaji wa sasa wa satalaiti unaendelea kuonyesha utulivu katika shughuli za nyuklia za nchi hiyo.
Matamshi hayo yametolewa wakati Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imetangaza kumalizika muda wa Azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambalo liliidhinisha makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015 na kuweka vikwazo ambavyo Tehran inasema muda wake umemalizika.