Je, kujenga vinu vya nyuklia kutaiwezesha Afrika au kutaimarisha utegemezi wa kigeni?
Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed mwezi uliopita alitangaza mipango ya kujenga vinu vya kwanza vya nyuklia nchini humo na hivyo kuashiria hamu kubwa ya bara la Afrika ya kumiliki nishati ya atomiki. Nchi za bara la Afrika zinahitaji kukidhi mahitaji ya nishati yanayoongezeka kila siku na kupunguza utegemezi wa nishati ya kisukuku.
Waziri Mkuu wa Ethiopia alitangaza mipango ya nchi hiyo ya kujenga vinu vya kwanza vya nyuklia mwezi jana wakati wa uzinduzi wa Bwawa la Grand Ethiopian Renaissance, kituo kikubwa zaidi cha kuzalisha umeme barani Afrika.
Ethiopia inalenga kuwa na vinu viwili vya kuzalisha umeme vya nyuklia kati ya mwaka 2032 na 2034; ambapo kila kinu kinatazamiwa kuzalisha takriban megawati 1,200 za umeme ili kuongeza uwezo wa sasa wa kuzalisha umeme kwa takriban asilimia 25.
Ethiopia mwishoni mwa Septemba mwaka huu ilitia saini makubaliano ya ushirikiano na Kampuni ya Russia ya Rosatom ili kuanza kutekeleza mradi wa ujenzi wa vinu vya nyuklia.
Afrika ina utajiri mkubwa wa urani, ambayo ni malighafi ya nishati ya nyuklia. Niger na Namibia pia ni miongoni mwa wazalishaji wakuu wa urani duniani, na Afrika Kusini pia ina akiba kubwa ya urani.
Hata hivyo, kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) ya mwezi Julai mwaka huu, Afrika Kusini ndiyo nchi pekee ya Afrika yenye mtambo wa nyuklia unaofanya kazi.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA); Misri imefika mbali ambapo sasa inajenga mtambo wa vitengo vinne. Kinu chacke cha kwanza inatarajiwa kukamilika ifikapo 2028.
Ghana, Kenya na Nigeria ziko katika awamu inayofuata, baada ya kuanzisha mamlaka za nyuklia na kuanza kazi ya maandalizi kwa ajili ya miradi ya baadaye.