Japan yapinga mashinikizo ya Marekani ya kuacha kununua nishati kutoka Russia
Yoji Muto, Waziri wa Biashara wa Japan amepinga vikali mashinikizo makubwa ya Marekani dhidi ya nchi hiyo. Marekani inaitaka Japan iache kununua nishati kutoka Russia. Tokyo, kwa upande wake, inasema kuwa itachukua maamuzi kwa mujibu wa maslahi yake ya kitaifa.
Muto ameeza haya kufuatia mkutano wa hivi karibuni kati ya Waziri wa Fedha wa Marekani, Scott Bessent na Waziri wa Fedha wa Japan, Katsunobu Kato, ambapo Bessent aliitaka Japan kusitisha kikamilifu ununuzi wa nishati kutoka Russia.
Huku akiafiki jitihada zinazoendelea kufanywa na Japan za kupunguza kwa kasi utegemezi wa nishati kutoka Russia tangu Moscow ianzishe operesheni ya kijeshi dhidi ya Ukraine mwezi Februari 2022, Muto amesisitiza kuwa Japan haitatii matakwa ya Washington.
Waziri wa Biashara wa Japan amesema gesi asilia (LNG) kutoka mradi wa Sakhalin-2 wa Russia bado ni muhimu, na kuongeza kuwa Japan inaagiza karibu asilimia 10 ya gesi hiyo asilia kutoka Russia na zalisha takriban asilimia 3 ya huduma ya umeme.
Amesisitiza kuwa mradi wa Sakhalin-2 wa Russia ni muhimu sana kwa usalama wa nishati wa Japan.
Marekani imezidisha jitihada za kupunguza mapato ya nishati ya Russia kwa kuwahimiza wanunuzi wakuu kama vile Japani, India na China wapunguze ununuzi wa nishati kutoka Russia. Washington inadai kuwa hatua kama hizo zingedhoofisha uwezo wa Moscow wa kuendeleza operesheni yake ya kijeshi nchini Ukraine.
Hata hivyo, takwa hili la Marekani limepingwa vikali na nchi nyingine huku China na india zikisema kuwa sera zao za kununua nishati kutoka Russia zinatekelezwa kwa mujibu wa maslahi yao ya kitaifa.
Wiki jana Mawaziri wa Nishati wa Umoja wa Ulaya pia walifikia makubaliano ya kutekeleza mpango uliokusudiwa kuzuia uuzaji nje mafuta ya Russia hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2027; hatua ambayo imeungwa mkono pakubwa na Washington.
Russia ni nchi ya tatu kwa uzalishaji wa mafuta baada ya Marekani na Saudi Arabia na muuzaji mkubwa wa gesi nje ya nchi.