Dec 08, 2025 02:30 UTC
  • Jumatatu, 08 Disemba, 2025

Leo ni Jumatatu, 17 Mfunguo Tisa Jamadithani 1447 Hijria sawa na 08 Disemba, 2025.

Siku kama ya leo miaka 923 iliyopita, yaani tarehe 17 Jamadithani mwaka 524 Hijiria, alifariki dunia Bari'i Baghdadi, mwanafasihi na malenga mashuhuri wa Kiarabu.

Baghdadi alizaliwa mwaka 443 Hijiria na kuanza kusomea elimu ya nahau na lugha kutoka kwa maulama wakubwa wa kipindi chake. Moja ya athari mashuhuri za Bari'i Baghdadi ni kitabu cha mashairi kilichopewa jina lake.

Malenga na mshairi huyo aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 81 hali akiwa ni kipofu.   

Miaka 860 iliyopita katika siku kama ya leo kulitiwa saini makubaliano ya kisiasa ya Acre katika kipindi cha Vita vya Msalaba baina ya Waislamu na wapiganaji wa Kikristo.

Makubaliano hayo yalitiwa saini kwa ajili ya kukabidhiwa mji wa Acre kwa Wakristo na mkabala wake kuachiliwa huru mateka wa Kiislamu wapatao 3,000. Hata hivyo na bila ya kuheshimu makubaliano hayo, Wakristo waliwaua mateka hao wa Kiislamu suala lililosababisha kuanza tena kwa Vita vya Msalaba ambavyo vilimalizika kwa kushindwa vibaya Wakristo.

Mji wa Acre ulikombolewa na Waislamu katika karne ya 15 Hijiria na ukachukuliwa tena na Wamagharibi mwaka 587. 

Siku kama ya leo miaka 157 iliyopita, ulianguka utawala wa Washugani au kwa jina jingine watawala wa kijeshi huko Japan.

Kuanguka kwa utawala huo kulipelekea kuanza kwa marekebisho ya kijamii, kisiasa na kiutamaduni nchini humo. Washugani walikuwa moja kati ya makumi ya silsila zenye nguvu huko Japan, walioanzisha utawala wao wa kidikteta tangu karne ya 12 Miladia. 

Katika siku kama ya leo miaka 127 iliyopita alifariki dunia msomi wa Kiislamu, Haj Mirza Hussein Nuri.

Msomi huyu mkubwa alifikia daraja ya juu katika ibada, ucha-Mungu na ukamilifu wa nafsi. Hajj Mirza Hussein alikuwa hodari katika elimu za fiqhi, Hadithi, tafsiri ya Qur'ani tukufu na mashairi, na likuwa mwandishi aliyebobea wa vitabu. Vitabu vyake vingi vilihusu elimu za Hadithi, tafsiri ya Qur'ani na ufafanuzi kuhusiana na maisha ya wasomi wa Kiislamu.

Mirza Hussein Nuri alilipa umuhimu mkubwa suala la kueneza athari za Ahlul-Baiti wa Mtume (saw). Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu ameandika vitabu vingi, na miongoni mwa athari zake mashuhuri ni kitabu cha "Mustadrakul Wasaail", "Maalimus Sabr", "Jannatul Maawa" na "Nafasur Rahman".

Mirza Hussein Nuri amezikwa katika mji mtakatifu wa Najaf nchini Iraq.

Katika siku kama ya leo miaka 122 aliaga dunia Herbert Spencer mwanafikra na mwanafalsafa wa Kiingereza.

Spencer alizaliwa mwaka 1820 na kujifunza elimu mbalimbali kutoka kwa baba yake. Alijiongezea ujuzi na elimu kutokana na juhudi zake za kupenda kutalii mambo mbalimbali.

Herbert Spencer aliamini kuwa, mtu anaweza kujipatia elimu kwa kushuhudia na kupata uzoefu. 

Miaka 111 iliyopita katika siku kama ya leo, vilijiri vita vya baharini vya Falkland pambizoni mwa visiwa vya Falkland katika Bahari ya Atlantic kati ya Uingereza na Ujerumani.

Vikosi vya wanamaji vya Ujerumani vilipigwa vibaya na vile vya Uingereza na visiwa hivyo vikatwaliwa tena na Waingereza. 

Visiwa vya Falkland ambavyo Argentina inasema ni milki yake, bado vinakaliwa kwa mabavu na Waingereza.

Siku kama ya leo miaka 76 iliyopita, Chian Kai-shek kiongozi wa wapigania uhuru wa China alikimbilia Taiwan akiwa na wafuasi wake wengi baada ya kushindwa na wapiganaji wa chama cha Kikomonisti chini ya uongozi wa Mao Tse Tung na akaunda serikali ya kitaifa ya Uchina.

Uungaji mkono wa Marekani kwa kiongozi huyo wakati huo ulipelekea Taiwan kujitenga na Uchina na kiti cha nchi hiyo katika Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama kikatolewa kwa Taiwan.

Hata hivyo mwaka 1971, kufuatia mazungumzo kati ya China na Marekani, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliitambua Jamhuri ya Watu wa China kwa kura nyingi, na nchi hiyo ilikubaliwa katika Baraza la Usalama, na hivyo Taiwan ikapokonywa uanachama katika Umoja wa Mataifa.