Jan 31, 2026 02:24 UTC
  • Leo Katika Historia
    Leo Katika Historia

Leo ni Jumamosi 11 Shaaban 1447 Hijria mwafaka na 31 Januari 2026 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1414 iliyopita, alizaliwa mtukufu Ali bin Hussein, maarufu kwa jina la Ali Akbar, mwana mkubwa wa kiume wa Imam Hussein (as) na mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) mjini Madina. Ali bin Hussein ambaye alifanana sana na babu yake, Mtume Mtukufu (saw), alinufaika na bahari ya maadili mema na mafunzo ya dini ya Kiislamu kwa kuwa pamoja na babu yake, Imam Ali (as), na baba yake, Imam Hussein (as). Ali bin Hussein alikuwa maarufu kwa jina la Ali al Akbar yaani Ali Mkubwa kutokana na jina lake kufanana na majina ya mdogo wake ambaye pia alikuwa na jina hilo la Ali. Ali Akbar alikuwa na nafasi muhimu katika mapambano ya baba yake dhidi ya dhulma za utawala wa Bani Umayyah. Aliuawa shahidi tarehe 10 Muharram mwaka 61 Hijiria baada ya kuingia katika medani ya vita na kupigana kishujaa katika mapambano ya jeshi la Yazid bin Muawiyah na Imam Hussein (as) na wafuasi wake. Siku ya kuzaliwa mtukufu huyo inatambiliwa nchini Iran kwa jina la Siku ya Vijana. 

Siku kama ya leo miaka 918 iliyopita alifariki dunia, Sanai Ghaznawi, malenga, tabibu na mwanairfani mkubwa wa Iran. Alizaliwa mwaka 467 Hijiria, na akiwa kijana mdogo alianza kusoma mashairi ya kuwasifu watawala. Hata hivyo muda mfupi baadaye aliachana na mwenendo huo na kuanza kusomea elimu ya irfan (ya kumjua Mwenyezi Mungu). Kuanzia wakati huo alianza kuishi maisha ya kuwatumikia wananchi sambamba na kutunga na kusoma mashairi ya kuwakosoa watawala dhalimu na mafisadi. Alianzisha pia mfumo wa aina yake katika kutunga mashairi.  Miongoni mwa athari za Sanai Ghaznawi ni pamoja na kitabu cha 'Hadiqatul-Haqiqah' ambacho kina muundo wa mashairi. Ndani ya kitabu hicho Ghaznawi ameweka wazi fikra zake za kiakhlaqi na irfani. Aidha vitabu vya 'Ilahi Nameh' 'Karnameh Balkh' na 'Twariqut-Tahqiq,' ni miongoni mwa athari za Sanai Ghaznawi. 

Siku kama ya leo miaka 427 iliyopita, ilianzishwa kampuni ya kwanza ya British East India Company nchini India kwa amri ya Malkia Elizabeth wa Kwanza wa Uingereza. Kampuni hiyo iliimarisha ukoloni wa Uingereza katika maeneo yenye utajiri huko kusini mwa Asia na baada ya hapo shughuli za ukoloni zikaimarika zaidi katika mataifa ya kusini mwa Asia kupitia kampuni hiyo. Baada ya kuasisiwa kampuni hiyo, nchi nyingine kama vile Uholanzi, Ureno na Ufaransa zilielekeza nguvu zao katika bara Hindi kwa lengo la kuhudumia ukoloni wao. Baada ya karne 3 za kuanzishwa kampuni hiyo, ushawishi na kuimarika utawala wa Uingereza nchini India vilisababisha nchi hiyo kutangazwa kuwa sehemu ya Uingereza, na Malkia Viktoria akavikwa taji la kuwa mtawala wa India na Uingereza. 

Miaka 377 iliyopita katika siku kama ya leo, Muhammad Taqi Majlisi mashuhuri kama Majlisi wa Kwanza alimu na msomi mkubwa wa Kiirani aliaga duunia. Alizaliwa 1003 Hijria katika mji wa Isfahan Iran katika kipindi ambacho mji huo ulikuwa mji mkuu wa utawala wa Safavi.  Familia ya Allama Majlisi yote ilifahamika kwa kushikamana na elimu. Allama Muhammad Taqi Majlisi bi miongoni mwa Maulamaa walio waliofanya safari kuelekea Najaf Iraq kwa ajili ya kujiendeleza kielimuu katika Hawza mashuhuri ya mji huo.  

Siku kama ya leo miaka 176 iliyopita, ilianzishwa harakati kubwa ya uasi ya wananchi wa China iliyokuwa ikijulikana kwa jina la Taiping. Harakati hiyo ilianzishwa kutokana na hali mbaya na umasikini uliokuwa ukiwasumbua wananchi wa nchi hiyo na hasa matabaka ya watu wa vijijini, iliyosababishwa na ukoloni wa kigeni na utawala wa familia isiyofaa ya Manchu. Lengo kuu la harakati hiyo iliyoendelea kwa muda wa miaka 14 lilikuwa ni kuhakikisha kunakuwepo usawa katika kugawana ardhi kati ya wanawake na wanaume.