Marekani yakiri wanajeshi wake wameuawa katika shambulizi la Iran nchini Jordan
-
CENTCOM imethibitisha wanajeshi wawili wa USA wameuawa katika mashambulizi ya Iran dhidi ya kambi ya kijeshi ya Marekani huko Jordan.
Jeshi la Marekani limethibitisha kwamba wanajeshi wake wasiopungua wawili wameuawa katika mashambulizi ya Iran yaliyolenga mali na kambi za kijeshi za za Marekani nchini Jordan.
Taarifa iliyotolewa na Kamandi Kuu ya Marekani (CENTCOM) imesema kwamba wanajeshi hao wawili waliuawa wakati wa mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani za Iran zilizolenga maeneo yanayodhibitiwa na Marekani huko Jordan juzi Julai 17.
CENTCOM imesema mwanajeshi mwingine mmoja ametoweka kufuatia mashambulizi ya Iran.
Taarifa hii ni ya kwanza ya aina yake tangu mapema mwezi huu, wakati Iran ilipoanza kushambulia kambi na vituo vya kijeshi vya Marekani katika eneo la Magharibi mwa Asia kujibu mashambulizi ya Washington katika maeneo ya pwani ya Iran kusini. Kwa kawaida, Marekani na washirika wake huficha na kujizuia kutangaza idadi ya wanajeshi wa nchi hiyo wanaoangamizwa katika mashambulizi ya Iran.
Wakati huo huo Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limeeleza kuwa limefanya mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya kambi ya kijeshi ya Marekani nchini Jordan, na kuharibu ndege kadhaa za kijeshi, huku likiwahimiza raia wa Jordan kupambana na vikosi vya jeshi la Marekani vilivyopo nchini humo.
Katika taarifa yake rasmi ya 29 iliyotolewa na Idara ya Uhusiano wa Umma siku ya Jumamosi, jeshi hilo lilisema kuwa Kikosi chake cha Anga kimetekeleza wimbi la 20 la Operesheni Nasr 2 ikiwa ni jibu kwa mashambulizi ya Marekani dhidi ya Iran yaliyofanyika usiku wa kuamkia jana Jumamosi.
Taarifa ya IRGC imesema, operesheni hiyo ililenga maeneo ya kuhifadhia ndege na eneo kubwa la kuegeshea ndege katika kituo cha kijeshi cha Marekani huko Azraq, mashariki mwa Jordan.
IRGC imeongeza kuwa shambulio hilo limeharibu ndege za kivita za Marekani zisizopungua mbili za Marekani na ndege nyingine tatu, na kusababisha uharibifu mkubwa kwa ndege nyingine katika kambi hiyo ya kijeshi ya Marekani huko Jordan.
Taarifa ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu imeongeza kuwa, Marekani inachochea na kupanua wigo wa vita kwa kulenga miundombinu ya kiraia ndani ya Iran ikiwemo hospitali, madaraja, reli, bandari na viwanja vya ndege.
"Washington inajaribu kuficha mapungufu na kushindwa kwake katika medani ya vita kwa kushambulia maeneo ya kiraia", imeeleza taarifa ya IRGC.
Ikiwahutubu wananchi na majeshi ya Jordan, taarifa hiyo imewataka kuchukua nafasi kubwa zaidi katika kukabiliana na jeshi la Marekani nchini humo, na kuonya kuwa wanajeshi wa kigeni wanaoendesha shughuli zao katika ardhi za Kiislamu ni shabaha halali chini ya mafundisho ya kidini ya wanazuoni wa Kiislamu kutoka madhehebu mbalimbali.
Taarifa hiyo iliwahimiza zaidi Wajordani kutumia "njia zote zinazowezekana" dhidi ya wanajeshi wa Marekani na kutoa wito wa kufukuzwa vikosi vya Marekani nchini Jordan, ikisisitiza kwamba Marekani inahusika na mauaji ya Waislamu katika nchi kadhaa, ikiwa ni pamoja na Afghanistan, Iraq, Iran, Yemen, Lebanon na Palestina.
Marekani Ijumaa usiku ilishambulia maeneo kadhaa katika mkoa wa kusini mwa Iran wa Hormozgan yakiwemo maeneo ya ndani na karibu na mji wa bandari wa Bandar Abbas, pamoja na miundombinu muhimu ya usafirishaji.