Baraza la Utawala Sudan: Hakuna mazungumzo na RSF huko Washington
-
Abdel Fattah al-Burhan
Baraza la utawala wa Mpito la Sudan limekanusha madai ya kuwepo mazungumzo yoyote ya moja kwa moja au yasiyo ya moja kwa moja na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) huko Washington, kama ilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari.
Baraza hilo limesema katika taarifa kwenye ukurasa wake wa jukwaa X: "Tunakanusha kabisa kile ambacho kimesambazwa katika baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kuhusu kuwepo mazungumzo ya moja kwa moja au yasiyo ya moja kwa moja kati ya Jeshi la Sudan na waasi (RSF) huko Washington."
Limesisitiza kwamba kinachosambazwa kuhusu suala hili "si kweli kabisa."
Taarifa hiyo imeongeza kuwa msimamo wa serikali uko wazi na thabiti kuhusu mazungumzo au suluhu yoyote, ambayo ni kujitolea kwake kwa suluhisho la kitaifa linalolinda uhuru wa nchi, umoja, utulivu na haki za watu wa Sudan.
Siku chache zilizopita, mkuu wa Baraza la Utawala wa Mpito, Abdel Fattah al-Burhan, alielezea nia yake ya kufanya mazungumzo kwa ajili ya maslahi ya Sudan na kukomesha vita kwa njia ambayo itarejesha umoja na heshima ya nchi hiyo.
Jeshi la Sudan limekuwa katika vita na waasi wa RSF tangu mwezi Aprili mwaka 2023 na hadi sasa zaidi ya 20,000 wameuawa na wengine milioni 14 wamelazimika kuwa wakimbizi kutokana na vita hivyo.