Jiji la Nairobi katika hatari ya kusombwa na mafuriko
Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa nchini Kenya imetoa onyo la mvua kubwa, katika maeneo kadhaa ya nchi, huku jiji la Nairobi likitajwa kuwa miongoni mwa maeneo yaliyo katika hatari kubwa ya kusombwa na mafuriko.
Katika utabiri wake unaohusu kipindi cha Oktoba 23 hadi Oktoba 30, wataalamu wa hali ya hewa wamesema kuwa sehemu za Bonde la Ziwa Victoria, Bonde la Ufa, na Nyanda za Juu Magharibi mwa Bonde la Ufa tayari zinaendelea kushuhudia mvua, lakini kiwango chake kinatarajiwa kuongezeka zaidi wiki ijayo.
Taarifa ya Idara ya Hali ya Hewa ya Kenya imesema, mvua hiyo inatarajiwa kuongezeka hadi zaidi ya milimita 30 ndani ya saa 24, na kusambaa hadi Nyanda za Juu Mashariki mwa Bonde la Ufa, ikiwemo Nairobi.
Kwa kuzingatia hali hiyo, Idara ya Hali ya Hewa ya Kenya imewahimiza wakazi wa maeneo yaliyoathiriwa kuwa waangalifu zaidi, kwani mvua hiyo kubwa huenda ikasababisha mafuriko ya ghafla na maporomoko ya ardhi, hasa katika maeneo ya tambarare na yenye milima.
Taarifa hiyo imeongeza: “Watu wanaoishi katika maeneo yanayokumbwa na hatari ya maporomoko ya ardhi, hususan kwenye miteremko ya Milima ya Aberdare, Mlima Kenya na maeneo yenye mteremko katika sehemu za magharibi, wanapaswa kuwa katika hali ya tahadhari.”
Ripoti zinasema katika jiji la Nairobi, hatari ni kubwa zaidi kutokana na mifumo duni ya kuondoa maji taka, hali inayofanya jiji hilo kuwa katika hatari ya mafuriko.