Ruto: Kuondolewa viza Afrika kutatatua changamoto za bara hilo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i131818-ruto_kuondolewa_viza_afrika_kutatatua_changamoto_za_bara_hilo
Rais William Ruto wa Kenya ameahidi kuongoza juhudi za kuondoa masharti ya viza kwa Waafrika na kutatua mizozo inayokumba bara hilo.
(last modified 2025-10-13T11:53:10+00:00 )
Oct 10, 2025 06:35 UTC
  • Ruto: Kuondolewa viza Afrika kutatatua changamoto za bara hilo

Rais William Ruto wa Kenya ameahidi kuongoza juhudi za kuondoa masharti ya viza kwa Waafrika na kutatua mizozo inayokumba bara hilo.

Rais Ruto alitoa ahadi hiyo jana Alkhamisi baada ya kupokezwa uenyekiti wa Jumuiya ya Soko la Pamoja la Afrika Mashariki na Kusini (COMESA) kutoka kwa Rais wa Burundi Évariste Ndayishimiye, wakati wa Kikao cha 24 cha Wakuu wa Nchi wa COMESA kilichofanyika jijini Nairobi.

Rais Ruto alisema kuwa, juhudi za kuunganisha Afrika haziwezi tu kuishia kwa mikataba ya kibiashara na masoko ya pamoja, bali ni lazima ziendelee hadi kufanikisha uhuru wa watu kusafiri, kufanya kazi, na kuwekeza kokote barani.

Kikao hicho cha COMESA kinachojumuisha wakuu wa nchi kutoka mataifa 21 wanachama ndicho chombo cha juu zaidi cha kufanya maamuzi katika jumuiya hiyo. Dakta Ruto ameuabmia mkutano huo kuwa, "Kuondolewa sharti la viza katika nchi za Afrika kutasaidia kupatia ufumbuzi changamoto za bara hilo."

Umoja wa Afrika ulipendekeza hivi karibuni kuwa, kuondolewa sharti la viza miongoni mwa wananchi wa bara Afrika ili kuzuru nchi za bara hilo, kutapunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya wananchi wa nchi za Kiafrika wanaoligura bara lao kwenda barani Ulaya kutafuta maisha bora.

Tayari nchi kadhaa za Afrika kama Kenya, Burkina Faso, Ethiopia, Gambia, Ushelisheli na Ghana zimetangaza kuondoa viza au malipo ya viza ya kuingia katika nchi hizo kwa Waafrika na wale wote wenye pasi za kusafria za Afrika.

Rwanda nayo inaruhusu raia wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) na Jumuiya ya Madola (Commonwealth), kupata viza bila malipo mara wanapowasili nchini humo, kwa ziara ya hadi siku 30.