Kagame: Nina matumaini mazungumzo yangu na Tshisekedi yatakuwa chanya
-
Kagame aonyesha matumaini chanya ya mazungumzo yajayo kati yake na Tshisekedi
Rais Paul Kagame wa Rwanda amesema ana matumaini kuwa, mazungumzo yaliyopangwa kufanyika Marekani kati yake na Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo yataleta matokeo chanya.
Rais Kagame amethibitisha mpango wa kukutana na kuzungumzia matumaini yake.
"Hata hatua ya kukubali kukutana mjini Washington ni kupiga hatua na bidii kubwa. Hatukufanya mambo hayo hapo kabla, tulipoteza muda mwingi bila kupiga hatua yoyote. Sasa nafikiri hii ni hatua muhimu inayoelekea pazuri na yenye matumaini kwamba tunakaribia amani ya kudumu jambo ambalo lazima tuendelee kuliunga mkono," alisema Paul Kagame.
Hata hivyo, katika mahojiano na wanahabari mjini Kigali, alielezea wasiwasi wake kuhusu nia ya viongozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, akisema kuwa siku za nyuma, wamekuwa na msimamo unaobadilika kuhusu walichokubaliana.
Akizungumzia kundi la waasi la FDLR linaloendesha harakati zake mashariki mwa Congo dhidi ya serikali ya Rwanda, Kagame kwa mara nyingine alimnyooshea kidole cha lawama Rais wa Congo kuwaunga mkono na ‘bila hata kuficha’.
Mwezi uliopita, Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo alimtaka tena mwenzake wa Rwanda Paul Kagame kuacha kuwasaidia waasi mashariki ya DRC na kutengeneza amani.
Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo imekuwa ikimtuhumu jirani yake Rwanda kuwa inaliunga mkono kundi la waasi wa M23, madai ambayo yamekanushwa na Kigali, lakini yanaungwa mkono na Marekani, Ufaransa, Ubelgiji na wataalamu wa Umoja wa Mataifa.