Makumi waaga dunia kwa mafuriko Indonesia, Thailand na Malaysia
-
Makumi ya watu wameaga dunia kwa janga la mafuriko Indonesia, Thailand na Malaysia
Kwa akali watu 250 wamefariki dunia katika mataifa ya Indonesia, Thailand na Malaysia kufuatia mvua kubwa iliyoambatana na mafuriko na maporomoko ya ardhi.
Mvua hiyo iliyoambatana na mfumo wa dhoruba za kitropiki imesababisha maafa katika maeneo mengi ya Indonesia, Thailand na Malaysia, na kusababisha wakazi kukwama kwenye mapaa ya nyumba.
Mafuriko makubwa na maporomoko ya ardhi yamesababisha vifo vya takriban watu 90 nchini Indonesia wiki hii huku mvua kubwa isiyo ya kawaida ikinyesha katika kisiwa cha Sumatra.
Kanda za video zinaonyesha mafuriko yakivunja kingo za mito, wakaazi wakiingia kwenye maji hadi kifuani, na magari na nyumba zikikaribia kuzama kabisa katika mitaa iliyofurika huku sehemu za paa zao zikiwa zimesalia tu kuonekana.
Wakati huo huo, Sri Lanka pia inakabiliwa na maafa mabaya zaidi ya hali ya hewa katika miaka ya hivi karibuni, na takriban watu 56 wamekufa na 21 hawajulikani walipo baada ya kutokea mafuriko na maporomoko ya ardhi katika maeneo kadhaa ya nchi.
Video zinazoonekana kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha nyumba zikisombwa na maji huku mafuriko yakipita mijini na huduma nyingi za treni zikifutwa kote nchini.
Mamlaka nchini Thailand, Malaysia, na Indonesia zinapambana kusaidia manusura wa mafuriko mabaya zaidi katika eneo hilo kwa miaka, ambayo yameathiri mamilioni na kuua watu wengi katika wiki iliyopita.
Serikali ya Thailand ilisema jana kuwa watu 55 hadi sasa wamekufa katika mafuriko kusini mwa nchi hiyo, ambayo yameathiri karibu watu milioni 3 na kuwapeleka maelfu katika vituo vya uokoaji.