Pezeshkian: Mlango wa diplomasia ungali wazi; awaonya maadui
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i128336-pezeshkian_mlango_wa_diplomasia_ungali_wazi_awaonya_maadui
Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian amesema Jamhuri ya Kiislamu inaamini kuwa dirisha la diplomasia bado liko wazi na kwamba nchi hii itatumia uwezo wake wote wa kisiasa kusonga mbele katika njia hii.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Jul 14, 2025 12:40 UTC
  • Pezeshkian: Mlango wa diplomasia ungali wazi; awaonya maadui

Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian amesema Jamhuri ya Kiislamu inaamini kuwa dirisha la diplomasia bado liko wazi na kwamba nchi hii itatumia uwezo wake wote wa kisiasa kusonga mbele katika njia hii.

"Tunatetea diplomasia na mwingiliano mzuri na tunapinga vita," Pezeshkian alisema hayo jana Jumatatu na kueleza kuwa, "Ili kuondoa kivuli cha vita katika nchi yetu, tutatumia rasilimali zote za kisiasa na kidiplomasia tulizo nazo wakati wa kutetea haki za asili za wananchi wa Iran." 

Ameongeza kuwa, Iran haijawahi kutaka kuanzisha vita lakini, badala yake imekuwa na nia ya kuwa na nafasi madhubuti katika kuhimiza amani ya kudumu duniani.

Rais wa Iran hata hivyo, amewatahadharisha maadui kwamba wakati taifa la Iran linatafuta amani, lakini haina maana ya kuwa dhalili na kujitweza.

"Kwa kuzingatia uhusiano wake wa kihistoria, kiutamaduni na kidini, Iran inatafuta haki na heshima kwa utu wa wanadamu wa mataifa yote," Pezeshkian amesisitiza.

Akiashiria uchokozi wa hivi karibuni wa Israel na Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu, Dakta Pezeshkian amesema adui Mzayuni aliishambulia Iran ilipokuwa katika mazungumzo na Marekani licha ya kutokuwa na imani na Wamarekani.

Ameongeza kuwa Tehran iliingia katika mazungumzo na Washington ili "kuondoa kutokuelewana katika mitazamo ya umma na kuthibitisha kuwa shughuli zake za nyuklia zina malengo ya amani."

Amekumbusha kuwa, wakati nchi hizo mbili zikifanya duru tano za mazungumzo na kupangwa kufanya mazungumzo mapya, utawala wa Israel, ukiungwa mkono na Marekani, uliishambulia Iran na kuua shahidi baadhi ya makamanda wa kijeshi wa Iran, wanasayansi wa nyuklia na raia, wakiwemo wanawake na watoto wasio na hatia.