Ansarullah yaionya Israel: Haiyumkiniki kufungua bandari ya Eilat
Kiongozi wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen ametangaza kuwa, ni jambo lisilowezekana kufunguliwa tena kwa bandari ya Eilat (Umm al-Rashrash), akisisitiza msimamo thabiti wa Yemen wa kuendelea kutekeleza vikwazo vya baharini dhidi ya utawala ghasibu wa Israel katika Bahari Nyekundu, Ghuba ya Aden na Bahari ya Arabia.
Katika hotuba yake kwa njia ya televisheni jana Alkhamisi, Abdul-Malik al-Houthi alisisitiza kwamba matukio ya hivi karibuni katika Bahari Nyekundu ni onyo la wazi kwa makampuni yote ya meli yanayofanya kazi kwa ajili ya utawala wa Israel na kusisitiza kwamba meli zozote zenye mfungamano na Israel zitakabiliwa na majibu madhubuti.
Alikuwa akizungumzia shambulio la jeshi la wanamaji la Yemen dhidi ya meli ya ETERNITY C kuelekea bandari ya Eilat iliyoko huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu, baada ya wafanyakazi hao kupuuza mara kadhaa maonyo ya askari wa Yemen.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, operesheni hiyo ya kijeshi ilifanywa kwa "chombo kisicho na rubani na makombora sita ya baharini na ya balestiki."
Kiongozi huyo wa Ansarullah ameeleza kuwa, jinai za Israel na uungwaji mkono inaopata kutoka kwa "Marekani na Magharibi havitaathiri kamwe msimamo wetu usioyumba katika kuiunga mkono Gaza."
Haya yanajiri huku vikosi vya Jeshi la Yemen vikiendelea kushambulia kwa kombora uwanja wa ndege wa Ben Gurion mjini Tel Aviv katika kuwaunga mkono Wapalestina wa Ukanda wa Gaza huku utawala wa kizayuni wa Israel ukiendeleza vita vya kinyama na mauaji ya kimbari dhidi ya eneo hilo uliloliwekea mzingiro.