Lebanon: Hatuna azma ya kuufanya wa kawaida uhusiano wetu na Israel
Rais Joseph Aoun wa Lebanon amesema nchi hiyo haina mpango wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel kwa sasa.
Matamshi hayo ya Rais Joseph Aoun ya jana Ijumaa yalikuja wakati utawala wa Donald Trump unajaribu kupanua 'Makubaliano ya Abraham' yaliyotiwa saini mnamo mwaka 2020, ambapo Israel ilitia saini mikataba ya kihistoria na Umoja wa Falme za Kiarabu na Bahrain, AP imeripoti.
Mwezi Mei mwaka huu, mtawala wa Syria, Ahmad al-Sharaa alisema katika ziara yake nchini Ufaransa kwamba, nchi yake inafanya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na Israel ili kuzuia shughuli za kijeshi kwenye mpaka wao kutoka nje ya udhibiti.
Mazungumzo kuhusu amani kati ya Israel na Syria yaliongezeka kufuatia kuondolewa madarakani kwa Rais Bashar Assad mwezi Disemba mwaka jana.
Rais Aoun ameongeza katika taarifa illiyotolewa na ofisi yake jana Ijumaa kwamba, ni taifa la Lebanon pekee litakalokuwa na silaha katika siku zijazo, na uamuzi wa iwapo Lebanon itaingia vitani au la utakuwa wa serikali ya Beirut.
Licha ya kufikiwa makubaliano ya kusitishwa mapigano na Lebanon, utawala wa Israel unaendelea kuishambulia nchi hiyo na kukiuka mamlaka yake.
Harakati ya Muqawama ya Hizbullah imeapa kwamba haitaweka silaha chini, wakati ambapo serikali ya Lebanon imechagua kunyamaza kutokana na hujuma za utawala ghasibu wa Israel.