Iran yaijia juu Marekani kwa kumwekea vikwazo Ripota wa UN
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i128210
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei ameikosoa vikali Marekani kwa kumwekea vikwazo Francesca Albanese, Ripota Maalum wa Umoja wa Mataifa katika ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
(last modified 2025-07-12T14:05:52+00:00 )
Jul 11, 2025 16:06 UTC
  • Iran yaijia juu Marekani kwa kumwekea vikwazo Ripota wa UN

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei ameikosoa vikali Marekani kwa kumwekea vikwazo Francesca Albanese, Ripota Maalum wa Umoja wa Mataifa katika ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

"Ukweli hauwezi kukandamizwa na vikwazo,” Baghaei amesema katika ujumbe alioutuma kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa X jana Ijumaa baada ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kumwekea vikwazo Francesca Albanese, mpelelezi huru wa Kiitaliano aliyepewa jukumu la kuchunguza ukiukwaji wa haki za binadamu katika maeneo ya Palestina.

"Francesca Albanese anaonewa na kuwekewa vikwazo kwa kusema ukweli na kusimama dhidi ya mauaji ya kimbari, uvamizi na ubaguzi wa rangi," amesema Baghaei.

"Wakati huo huo, Netanyahu, mhalifu wa vita aliyethibitishwa na mahakama, anawekewa zulia jekundu huko (Washington) DC", Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran amebainisha. "Unafiki wenu unaanikwa wazi, huku ulimwengu ukitazama," Baghaei amewahutubu maafisa wa Marekani.

Kabla ya hapo, aliyekuwa Makamu wa Rais katika Masuala ya Kistratajia wa Iran, Mohammad-Javad Zarif pia alikosoa hatua hiyo ya Marekani ya kumuwekea vikwazo Francesca Albanese, Ripota Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya haki za binadamu katika Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Gaza, huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Jumatano iliyopita, waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Marco Rubio alitoa tamko la serikali kwa kusema: "Leo ninaweka vikwazo kwa Ripota Maalumu wa Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa, Francesca Albanese kwa hatua zake zisizo halali na za kuaibisha kutaka Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ichukue hatua dhidi ya maafisa wa Marekani na Israel, makampuni na watendaji".