Mataifa yaliyokutana Bogota, yatangaza hatua 6 ‘madhubuti’ yatazochukua dhidi ya Israel
Muungano wa mataifa mbalimbali duniani yaliyokutana Bogota, mji mkuu wa Colombia umekubaliana kutekeleza hatua sita za kukomesha mashambulizi ya utawala wa kizayuni wa Israel dhidi ya Ghaza na kuzuia ukiukaji wa sheria za kimataifa unaofanywa na utawala huo haramu.
Hatua hizo ni pamoja na kuzuia usafirishaji wa silaha na zana za kijeshi unazopelekewa utawala wa kizayuni wa Israel.
Tangazo la makubaliano hayo limetolewa baada ya "mkutano wa dharura" ulioandaliwa kwa pamoja na serikali za Colombia na Afrika Kusini kama wenyeviti wenza wa Kundi la The Hague, ili kuratibu hatua za kidiplomasia na za kisheria kukabiliana na kile wanachoelezea kama "kinga ya kutofuatiliwa kisheria" inayowezeshwa na Israel na washirika wake wenye nguvu.
Kundi la The Hague kwa sasa ni kambi ya mataifa manane, iliyozinduliwa tarehe 31 Januari katika mji huo wa Uholanzi, kwa lengo lililowekwa la kuiwajibisha Israel chini ya sheria za kimataifa.
Mkutano huo ulileta pamoja zaidi ya mataifa 30, ikiwa ni pamoja na Algeria, Bolivia, Botswana, Brazil, Chile, China, Cuba, Djibouti, Honduras, Indonesia, Iraq, Ireland, Lebanon, Libya, Malaysia, Mexico, Namibia, Nicaragua, Norway, Oman, Pakistan, Palestina, Ureno, Uhispania, Qatar, Uturuki, Slovenia, Saint Vincent na Grenadini, Uruguay, na Venezuela.
"Tumekuja Bogota kuweka historia - na tumeiweka," ameeleza Rais wa Colombia Gustavo Petro.
Katika hotuba ya ufungaji wa mkutano huo, Francesca Albanese, ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia hali ya haki za binadamu katika ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu, amesema: "hizi si hatua tu bali ni njia za kuokoa maisha ya watu ambao wanakabiliwa na mashambulio yasiyokoma na ulimwengu ambao umepooza kwa muda mrefu."
"Mataifa haya 12 yamepiga hatua kubwa," amebainisha Albanese na kuongezea kwa kusema: "muda sasa unayaelekea mataifa mengine, kutoka Ulaya hadi ulimwengu wa Kiarabu na kwingineko, ili kuungana nayo"…/