Intelijensia: US inajifanya inataka kuzungumza na Iran wakati inajiandaa kwa vita
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i128462
Afisa mmoja mwandamizi wa kisiasa wa Iran ameiambia Press TV kuwa Jamhuri ya Kiislamu haitaingia kwenye mazungumzo mapya na Marekani kwa kutumia mfumo au ajenda ya hapo awali, baada ya funzo ililopata kutokana na mazungumzo ya hapo kabla.
(last modified 2025-07-18T14:06:20+00:00 )
Jul 18, 2025 05:09 UTC
  • Intelijensia: US inajifanya inataka kuzungumza na Iran wakati inajiandaa kwa vita

Afisa mmoja mwandamizi wa kisiasa wa Iran ameiambia Press TV kuwa Jamhuri ya Kiislamu haitaingia kwenye mazungumzo mapya na Marekani kwa kutumia mfumo au ajenda ya hapo awali, baada ya funzo ililopata kutokana na mazungumzo ya hapo kabla.

Afisa huyo ambaye ameomba kutotajwa jina, amesisitiza kwamba mazungumzo yoyote lazima yaendane na hali halisi ya kiusalama ya eneo.

"Kwa sasa, tunadhani lengo la mazungumzo hayo ni kuipokonya Iran silaha ili kufidia udhaifu wa Israel katika vita vijavyo," amebainisha afisa huyo.

"Intelijensia yetu inaonyesha kuwa Washington inataka mazungumzo ili kujiandaa kwa vita, na si amani. Kama ni hivyo, hatuoni sababu ya kupoteza muda, bali tunahisi ni bora kujiandaa kwa makabiliano."

Afisa huyo ameongeza kuwa duru yoyote mpya ya mazungumzo lazima ijumuishe utoaji "dhamana za maana na za kivitendo" ili kuhakikisha mchakato huo hauwi kisingizio cha kufanyia udanganyifu wa kiusalama.

Afisa huyo ameiambia Press TV kwamba masharti muhimu ya mazungumzo, inapasa yawe ni pamoja na kufuatiliwa kwa uzito mkubwa mpango wa nyuklia wa utawala wa kizayuni wa Israel na silaha zake za maangamizi.

"Hakuna mtu yeyote katika eneo atakayekubali ufanyike upokonyaji silaha katika eneo hili wakati utawala mwagaji damu unazidi kuzatitiwa kwa silaha kila siku"…/