Ripoti: Mienendo ya Netanyahu inaitia wasiwasi White House
Baadhi ya maafisa wakuu wa Marekani wameliambia shirika la habari la Axios kwamba, hofu inaongezeka ndani ya utawala wa Donald Trump juu ya tabia na mienendo ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, wakielezea mienendo hiyo kama ya kutojali, kuvuruga uthabiti, na wakati mwingine yenye ukosefu wa ukomavu.
"Hisia kwamba kidole cha Netanyahu daima kipo kwenye kitufe imekuwa ya kusumbua sana," afisa mmoja wa Marekani aliiambia Axios na kuongeza kwamba, baadhi ya mienendo ya Netanyahu imeonekana kuwa "ya kitoto na isiyofaa."
Afisa mwingine mkuu wa Marekani ambaye hakutaka jina lake lijtajwe ameashiria mashambulizi ya karibuni ya Israel dhidi ya Syria na kueleza kuwa: Israel "haipaswi kuwa ndiyo yenye maamuzi ya iwapo serikali ya Syria inaweza kuwa na mamlaka juu ya eneo lake au la.
Aidha afisa mmoja wa Israel ambaye pia jina lake halikutajwa ameonya kwamba, mkakati wa sasa wa Tel Aviv unaweza "kuyumbisha zaidi Syria," na hatimaye kuwadhuru walowezi wa Israel na jamii ya Druze.
Licha ya kusimamishwa kwa muda kwa mashambulizi ya Israel ndani ya Syria, vyanzo vya Axios vinasema wasiwasi ndani wa Marekani juu ya kushadidi kwa taharuki katika eneo kunakochochewa na Netanyahu, unaongezeka.
Kadhalika afisa mwingine amesema mashambulio ya kushtukiza ya hivi majuzi la Israel nchini Syria "yalimtia wahaka Rais Trump na washauri wa White House."
Kwa mujibu wa Axios, Trump akiashiria hujuma za Israel nchini Russia, alieleza kutofurahishwa na kutazama nchi ambayo ipo "kwenye njia ya kuelekea kwenye amani" ikipigwa mabomu.