Papa ‘ashambuliwa’ kwa msimamo wake kuhusu kushambuliwa kanisa Ghaza
Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Leo anaandamwa na ukosoaji mkali kutokana na mjibizo aliotoa kuhusiana na shambulio la anga lililofanywa na utawala wa kizayuni wa Israel dhidi ya kanisa pekee la Kikatoliki katika Ukanda wa Ghaza.
Shambulio hilo lililofanywa siku ya Alkhamisi iliyopita, liliua watu watatu na kujeruhi wengine kadhaa, akiwemo mchungaji.
Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni alilaani shambulio hilo na akasema "mashambulio dhidi ya raia ambayo Israel imekuwa ikifanya kwa miezi kadhaa hayakubaliki".
Hata hivyo katika taarifa yake, Papa Leo alionyesha masikitiko tu na kutoa wito wa amani, lakini akaacha kuitaja Israel kama mhusika wa jinai hiyo, na hivyo kuibua hasira na ukosoaji mkali kutoka kwa Wakristo wa Palestina na wafuatiliaji wa mambo duniani kote.
Katika ujumbe wake, Kiongozi huyo wa Wakatoliki aliandika: "nimehuzunishwa sana kwa kupata habari kuhusu (watu) kupoteza maisha na kujeruhiwa kulikosababishwa na shambulio la kijeshi dhidi ya Kanisa Katoliki la Familia Takatifu huko #Gaza. Ninaipa hakikisho jamii ya parokia ukaribu wangu wa kiroho. Nazifariji roho za marehemu kwa rehema za upendo za Mwenyezi Mungu, na kuombea familia zao na majeruhi. Ninarudia wito wangu wa kusitishwa vita mara moja. Ni mazungumzo na maridhiano tu ndiyo yatakayoleta amani ya kudumu!”
Kufuatia kauli hiyo ya Papa, watumiaji wa mitandao ya kijamii wametaka utolewe wito wa uwazi zaidi wa uwajibikaji kwa utawala wa kizayuni.
Mtumiaji mmoja amelikosoa tamko la Papa Leo akisema, taarifa hiyo ni "jibu la kuaibisha".
Mwingine akasema: "Wakristo wa Ghaza hawateseki kwa sababu wameshindwa kujitolea kwa ajili ya 'mazungumzo na maridhiano".
Watumiaji wengi wa mitandao ya kijamii wamemlinganisha Papa Leo na mtangulizi wake Papa Francis aliyekuwa akiilaani na kuikosoa waziwazi Israel kwa jinai zake, na kuonyesha kusikitishwa na jibu lililotolewa na Papa huyo mpya.
Utawala wa kizayuni wa Israel umekaribisha na kuridhishwa na kauli ya Papa.".../