Rais wa Eritrea aitahadharisha Ethiopia juu ya kuibuka mzozo mpya
-
Isaias Afwerki
Rais wa Eritrea, Isaias Afwerki, ametoa tahadhari kwa jirani yake Ethiopia, na kuonya juu ya uwezekano wa kuzuka mzozo mpya kati ya nchi mbili huku hali ya wasiwasi ikiongezeka katika eneo la Pembe ya Afrika.
Uhusiano kati ya nchi mbili hizi jirani umesalia kuwa tete tangu Eritrea ilipojitenga na Ethiopia mwaka 1993. Vita vya umwagaji damu vya mpakani vilivyojiri kuanzia mwaka 1998 hadi 2000 vilisababisha vifo vya makumi ya maelfu ya watu.
Eritrea na Ethiopia pia zimeendelea kutoamiania licha ya kusaini makubaliano ya amani mwaka 2018.
Serikali ya Eritrea inasema kuwa, vuta nikuvite inayoshuhudiwa sasa inasababishwa na mwelekeo mpya wa Ethiopia wa kutaka kuwa na bandari.
Rais Isaias Afwerki wa Eritrea ametoa matamshi hayo aliyoyaelekeza kwa Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed akitahadharisha kuwa Eritrea haitazidiwa nguvu kwa urahisi na jamii kubwa ya watu wa Ethiopia wanaokadiriwa kuwa milioni 130 mkabala wa jamii ya watu milioni tatu na laki tano ya wananchi wa Eritrea.
Rais wa Eritrea amesisitiza kuwa nchi yake iko tayari kujihami yenyewe iwapo italazimika kufanya hivyo.