Majeshi ya Iran yaonya kuhusu jibu kwa tishio lolote la Israel
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i139450-majeshi_ya_iran_yaonya_kuhusu_jibu_kwa_tishio_lolote_la_israel
Kamandi Kuu ya Majeshi ya Iran imeonya kwamba Jamhuri ya Kiislamu itajibu “hatua hatari” za Israel katika anga za baadhi ya nchi jirani.
(last modified 2026-06-27T03:06:55+00:00 )
Jun 27, 2026 03:01 UTC
  • Majeshi ya Iran yaonya kuhusu jibu kwa tishio lolote la Israel

Kamandi Kuu ya Majeshi ya Iran imeonya kwamba Jamhuri ya Kiislamu itajibu “hatua hatari” za Israel katika anga za baadhi ya nchi jirani.

Kamandi ya Khatam al-Anbiya imesema katika taarifa iliyotolewa siku ya Ijumaa kwamba: “Tunaona mienendo na uwepo wa ndege za kijeshi za utawala wa Kizayuni na wa kigaidi katiika anga ya baadhi ya nchi jirani kuelekea Iran kuwa ni kitendo hatari na tishio dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran,”

Taarifa hiyo imesisitiza kwamba: “Iwapo Marekani haiwezi kuuzuia na kuudhibiti utawala wa Kizayuni, basi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitavumilia tishio lolote na inaona kuwa ni haki yake kujibu hatua hizo hatari.”

Iran pia imetoa onyo rasmi la mwisho kwa serikali ya Iraq na Serikali ya Mkoa wa Kurdistan wenye mamlaka ya kujitawala (KRG), ikizitaka kuchukua hatua za haraka dhidi ya makundi ya kigaidi yanayoipinga Iran yaliyojikita kaskazini mwa Iraq.

Ujumbe huo, uliowasilishwa kupitia Balozi wa Iraq mjini Tehran, Yasser al-Hajjaj, umezipa Baghdad na Erbil machaguo mawili: kuwakamata vinara wa makundi hayo na kuwarejesha Tehran ili wafunguliwe mashtaka kutokana na harakati zao za kigaidi, au kuwezesha kuhamishwa kwao kwenda nchi ya tatu ndani ya muda maalumu.

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, Tehran imeweka wazi kwamba inakutambua kuendelea harakati za makundi hayo katika eneo la Kurdistan la Iraq kuwa ni tishio la moja kwa moja kwa usalama wake wa kitaifa, na inatarajia jibu la wazi na la kivitendo kutoka kwa serikali ya shirikisho ya Iraq pamoja na mamlaka za Kikurdi.

Vikosi vya majeshi ya Iran vimefanya mashambulizi ya mara kwa mara katika miezi ya karibuni, ikiwemo operesheni ya tarehe 8 Juni iliyolenga makao makuu ya kundi la kigaidi mjini Sulaymaniyah. Tehran tayari imeonya kwamba ikiwa makundi yanayotaka kujitenga yataruhusiwa kuingia Iran kutoka eneo hilo, basi miundombinu yote katika eneo la Kurdistan la Iraq italengwa kwa mashambulizi makubwa.

Marekani ilikuwa imeandaa mpango wa kuivamia Iran kwa njia ya nchi kavu kwa kushirikisha makundi yenye silaha ya Kikurdi katika maandalizi ya vita vya siku 40, lakini operesheni hiyo haikutekelezwa kamwe. Hayo ni mujibu wa mwandishi mwandamizi wa BBC Persian, Jiyar Gol, aliyeripoti siku ya Alhamisi akinukuu vyanzo kadhaa.

Maafisa wa Marekani waliwaarifu wakuu wa vyama vya Kikurdi vya Iraq kabla ya uchokozi huo kuanza kwamba shambulio dhidi ya Iran limekaribia, na kwamba makundi hayo yangetarajiwa kushambulia vituo vya Iran pamoja na maeneo ya usalama katika mipaka ya nchi mbili iwapo mapigano yangeanza.

Hata hivyo, operesheni hiyo haikufanyika, baada ya Trump kuamua kutofuatilia mpango huo. Kwa muda mrefu, Israel imeendelea kuwa na uhusiano wa kijeshi, kijasusi na kibiashara kwa njia za siri na makundi ya Kikurdi yanayotaka mkoa wa Kurdistan ujitenge na Iran.

Shirika la ujasusi la Mossad limeanzisha vituo vya kijasusi na kiutendaji ndani ya eneo la Kurdistan la Iraq, na wanamgambo wa Kikurdi wanadaiwa kufadhiliwa na Mossad pamoja na CIA.