Nchi tatu za Muungano wa Sahel zazindua kitambulisho cha pamoja
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i128518-nchi_tatu_za_muungano_wa_sahel_zazindua_kitambulisho_cha_pamoja
Katika hatua mpya ya umoja wa kanda, Muungano wa Mataifa ya Sahel, AES, umetangaza uzinduzi wa kadi ya utambulisho ya pamoja inayotumia teknolojia ya kibiometri.
(last modified 2025-07-19T23:00:00+00:00 )
Jul 19, 2025 23:00 UTC
  • Nchi tatu za Muungano wa Sahel zazindua kitambulisho cha pamoja

Katika hatua mpya ya umoja wa kanda, Muungano wa Mataifa ya Sahel, AES, umetangaza uzinduzi wa kadi ya utambulisho ya pamoja inayotumia teknolojia ya kibiometri.

Lengo la mpango huu ni kurahisisha usafiri huru wa watu ndani ya mazingira ya usalama ya Sahel, kama alivyoeleza Waziri wa Usalama wa Mali, Daoud Aly Mohammedine.“Kadi ya utambulisho ya AES itaanza kutumika hivi karibuni,” alitangaza bila kuweka tarehe maalum ya kuanza. Kadi hii inaashiria ahadi ya pamoja ya Mali, Niger, na Burkina Faso ya kurahisisha usafiri wa raia wao ndani ya eneo lao la ushirikiano.

Mradi huu ulipitishwa rasmi katika mkutano wa mawaziri uliofanyika Bamako Novemba iliyopita. 

Muungano wa Mataifa ya Sahel  ulianzishwa rasmi Septemba 2023 na Burkina Faso, Mali, na Niger kama mkataba wa pamoja wa ulinzi na ushirikiano baada ya kuondolewa kwa wanajeshi wa Ufaransa katika mataifa hayo. Tangu wakati huo, nchi hizo zinazoongozwa na serikali za mpito za kijeshi zimejiondoa kutoka jumuiya ya ECOWAS, zikiitaja kuwa chombo cha ushawishi wa mkoloni wa zamani, Ufaransa, na tishio kwa uhuru wao.

Muungano wa Mataifa ya Sahel umejiweka kama upinzani thabiti dhidi ya ushawishi wa Magharibi katika ukanda wa Sahel, hususan dhidi ya mkoloni mkongwe, Ufaransa. Kikundi hicho pia kimesitisha ushirikiano wa kijeshi na washirika wao wa zamani wa Ulaya na Marekani na kuelekeza ushirikiano zaidi kwa Russia na washirika wengine wa nje ya ulimwengu wa Magharibi.

Rais wa Burkina Faso, Kapteni Traoré, ameonya kuwa juhudi za Magharibi za kuichafua Sahel zinaendeshwa na tamaa ya rasilimali lukuki za asili ambazo bado hazijagunduliwa wala kutumika ipasavyo.