Kiongozi wa Hizbullah: Israel italazimika kuondoka Lebanon “ikiwa imedhalilika”
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i139448-kiongozi_wa_hizbullah_israel_italazimika_kuondoka_lebanon_ikiwa_imedhalilika
Katibu Mkuu wa Hizbullah, Sheikh Naim Qassem, amesema kuwa Israel italazimika kuondoka bila masharti katika kila sehemu ya ardhi ya Lebanon, ikiwa “imeshindwa na kudhalilika.”
(last modified 2026-06-27T03:01:26+00:00 )
Jun 27, 2026 02:59 UTC
  • Sheikh Naim Qassem
    Sheikh Naim Qassem

Katibu Mkuu wa Hizbullah, Sheikh Naim Qassem, amesema kuwa Israel italazimika kuondoka bila masharti katika kila sehemu ya ardhi ya Lebanon, ikiwa “imeshindwa na kudhalilika.”

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Ashura katika vitongoji vya kusini mwa Beirut siku ya Ijumaa, Sheikh Qassem amesisitiza tena kwamba Israel lazima ikomeshe operesheni zake za kijeshi za nchi kavu, angani na baharini, na iondoke kikamilifu katika ardhi ya Lebanon.

Amesema: “Israel haina chaguo ila kuondoka kikamilifu katika ardhi yetu." Aidha amepinga mpango wowote ambao utairuhusu Israel kubaki ndani ya Lebanon au kuwepo uhusiano wa kawaida kati ya Beirut na Tel Aviv.

Lebanon na Israel kwa sasa ziko katika mazungumzo yanayoratibiwa na Marekani, yakilenga miongoni mwa mambo mengine kuhakikisha Israel inaondoka kusini mwa Lebanon.

Wakati duru mpya ya mazungumzo ilifanyika Washington siku ya Jumanne, Rais wa Lebanon, Joseph Aoun alisisitiza tena kwamba Beirut haitakubali kitu chochote kilicho chini ya kumalizika kikamilifu uvamizi wa Israel kusini mwa Lebanon.

Hata hivyo, maafisa waandamizi wa Israel wamesema kuwa wanajeshi wa utawala huo watabaki kusini mwa Lebanon kwa muda usiojulikana.

Kiongozi huyo wa Hizbullah amesema kuwa kukataa kwa Israel kuondoka kwenye ardhi ya Lebanon ni sehemu ya mradi mpana zaidi wa uvamizi na akaonya kwamba Lebanon haitakubali mpangilio wowote unaodhoofisha mamlaka yake ya kitaifa.

Akiwahutubia viongozi wa kisiasa wa Lebanon, Sheikh Qassem ametoa wito wa ushirikiano unaojengwa juu ya mamlaka ya taifa, akisema kwamba Hizbullah iko “tayari na inanyoosha mkono” kufanya kazi pamoja na serikali ili kuhakikisha Israel inaondoka kikamilifu katika ardhi ya Lebanon.

Amengeza kuwa “muqawama una nguvu, na sisi tuko pamoja nanyi ikiwa mtaendelea katika njia ya mamlaka ya Lebanon.”

Sheikh Qassem pia amesema kuwa hati ya makubaliano ya maelewano (MoU) iliyotiwa saini hivi karibuni kati ya Iran na Marekani inatoa fursa kwa mamlaka za Lebanon kuimarisha mamlaka ya nchi hiyo.

Akiyataja makubaliano hayo kuwa ni “tamko rasmi la kushindwa kwa Marekani na Israel,” Sheikh Qassem amesema kuwa Iran sasa ina mchango mkubwa katika kuunda mustakabali wa eneo hili.

Amesema kuwa “nguvu ya Iran, pamoja na nguvu ya wapiganaji wa muqawama… husaidia kuleta uwiano unaohitajika ili kuivunja Israel na kuifukuza kutoka ardhi yetu.”

Iran imeendelea kusisitiza kwamba Lebanon ni sehemu muhimu ya makubaliano ya awali yaliyotiwa saini na Washington, huku ikionya kwamba itachukua hatua zote zinazohitajika kulinda maslahi yake, usalama wake na haki zake, pamoja na zile za washirika wake.