Ahmadian: Iran inapinga mabadiliko yoyote ya kijiopolitiki katika eneo
Ali Akbar Ahmadian Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran (SNSC) amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu inapinga vikali mabadiliko yoyote ya kijiopolitiki katika eneo la Magharibi mwa Asia.
Ali Akbar Ahmadian alieleza haya jana katika mazungumzo ya simu na Armen Grigoryan Katibu wa Baraza la Usalama wa Taifa la Armenia. Amesema kuwa Tehran inaamini kuwa mataifa yote ya kanda hii yananufaika na sera hii.
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran pia amepongeza msimamo wa Armenia wa kulaani uvamizi wa Israel dhidi ya Iran katika vita vya siku 12 vilivyoanzishwa na utawala huo ghasibu dhidi ya taifa hili.
Katika mazungumzo yao ya simu, Ahmadian na Grigoryan wamejadli masuala ya pande mbili na ya kikanda. Kwingineko, afisa huyo wa Armenia amemweleza mwenzake wa Iran kuhusu mazungumzo ya karibuni kati ya Armenia na Azerbaijan na kusisitiza juu ya msimamo usiobadilika wa Yerevan kuhusiana na masuala ya korido za kikanda za usafirishaji.
Itakumbukwa kuwa, mwezi Mei mwaka huu Armenia na Azerbaijan zilikubaliana kuhusu rasimu ya makubaliano ya amani ili kuhitimisha mzozo wa karibu miongo minne kati ya nchi za Kaukazia ya Kusini huku serikali ya Yerevan ikikubali kusalimu amri mkabala wa madai yake kwa Karabakh.
Eneo la Karabakh ambalo liliathiriwa na mgogoro wa muda mrefu lilikuwa kitovu cha vita vya gharama kubwa kati ya Armenia na Azerbaijan mwaka 1990 na 2020.
Eneo la Karabakh limekuwa likitambuliwa kimataifa kama sehemu ya Azerbajan.