Iran: Hatutaachana na haki yetu ya kurutubisha urani
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu haina nia ya kuachana na mpango wake wa nyuklia, ikiwemo kurutubisha madini ya urani, licha ya uvamizi wa kijeshi wa mwezi uliopita wa Marekani na mutifaki wake wa kieneo, Israel.
Katika mahojiano na runinga ya Fox News ya Marekani jana Jumatatu, Abbas Araghchi amesema kuwa, ni wazi Iran "hatutaacha kurutubisha urani kwa sababu ni mafanikio ya wanasayansi wetu" na chanzo cha fahari ya kitaifa.
Alipoulizwa iwapo kuna madini yoyote ye urani iliyorutubishwa ambayo yamehifadhiwa kutokana na mashambulizi ya Marekani, Araghchi amesema "hakuwa na taarifa za kina," lakini akabainisha kuwa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran "linajaribu kutathmini ni nini hasa kilitokea kwa taasisi zetu za nyuklia, na kwa madini yaliyorutubishwa."
Rais wa Marekani Donald Trump amekuwa akidai kuwa, shambulio la Marekani dhidi ya taasisi za nyuklia za Iran lilikuwa la mafanikio, na kukariri Jumamosi madai hayo kwamba maeneo yote matatu yaliyolengwa "yaliharibiwa kikamilifu."
Kuhusu mazungumzo na Marekani, Araghchi ameeleza kuwa Tehran iko tayari kwa majadiliano lakini haina mpango wa mazungumzo ya moja kwa moja na Washington kwa wakati huu.
Amebainisha kuwa, Iran iko tayari kuchukua hatua zozote zinazohitajika kujenga muamana, ili kuthibitisha kwamba mpango wake wa nyuklia ni wa amani, makabala wa kuondolewa vikwazo vya Marekani, huku akisisitiza kwamba makubaliano yoyote ya baadaye ya nyuklia lazima yajumuishe haki ya Iran kurutubisha urani.
Weledi wa mambo wanasisitiza kuwa, hatua ya Iran kurutubisha madini ya urani hadi kiwango cha asilimia 60 ni mjibizo kwa vikwazo na mashinikizo ya kimataifa inayowekewa.