Onyo la Iran kwa Marekani; Usirudie tena vita vilivyofeli vya siku 12
Tehran imemuonya Rais Donald Trump wa Marekani kuhusu kukariri uzoefu uliofeli wakati wa vita vya siku 12 vya utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran.
Seyyed Abbas Araghchi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mahojiano na Fox News amemuonya Rais wa Marekani kutorudia kosa alilofanya mwezi Juni uliopita. Araghchi, akijibu swali kuhusu ujumbe alionao kwa kwa Trump amesema: "Usirudie kosa ulilofanya mwezi Juni. Unajua kwamba ukikariri jaribio hilo lililofeli, utapata matokeo yale yale uliyopata wakati uliopita. Uliharibu vifaa na mashine (za nyuklia), lakini huwezi kulipua teknolojia, nia na azma kwa mabomu. Araghchi amesisitiza kuwa: Tulikabiliwa na operesheni kubwa ya kigaidi mnamo Januari 8-10, na tunalichukulia hili kuwa mwendelezo wa vita vya siku 12 vya Marekani na utawala wa Israel dhidi yetu. Yaani, tarehe 8 Januari ilikuwa siku ya 13 ya vita hivyo."
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alifafanua kuhusu matukio ya hivi karibuni kwa kusema: 'Jambo lililopelekea magaidi kuwapiga risasi raia ni kwa sababu walitaka kumuingiza Trump vitani. Israel inataka Marekani iingie vitani na Iran kwa niaba ya utawala huo, na lengo hili la siri la Tel Aviv sasa limefichuka." Ameendelea kusema: "Kuongezeka kwa mvutano kutakuwa na matokeo mabaya kwa kila mtu. Operesheni hiyo ya kigaidi iliyotekelezwa kwa muda wa siku tatu ilikuwa mwendelezo wa vita vya siku 12 ambavyo Marekani na Israel ziliviendesha dhidi yetu." Araghchi ameendelea kusema kuwa, Wamarekani kurudia uzoefu uliofeli hakutawaletea matokeo tofauti na kusisitiza kuwa Iran siku zote imekuwa tayari kwa mazungumzo na diplomasia.
Onyo la Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran kwa rais mwenye utata mwingi wa Marekani la kumtaka aepuke kukariri uzoefu uliofeli wa vita vya siku 12 vya Israel dhidi ya Iran linatokana na msururu wa mazingatio ya kistratejia, kisiasa na kiusalama ambayo yanaakisiwa waziwazi katika maneno yake. Katika mazungumzo yake ya hivi karibuni, Araghchi alisisitiza kuwa Iran iko katika kiwango cha juu zaidi cha utayarifu wa kijeshi kuliko ilivyokuwa wakati wa vita vya siku 12 mwaka jana, na kwamba hatua yoyote ya kijeshi ya Marekani au washirika wake itakabiliwa na jibu kali na la gharama kubwa kwa adui. Onyo hili sio msimamo wa kihemko tu, bali ni ujumbe uliotathminiwa vizuri kwa ajili ya kuzuia Marekani kuingia kwenye njia ambayo tayari imekwishaona matokeo yake.
Sababu ya kwanza ya onyo hili ni kushindwa wazi kwa operesheni ya pamoja ya Marekani na Israel katika vita vya siku 12 vya mwaka uliopita. Operesheni hiyo ambayo ilitekelezwa kwa lengo la kuvunja uwezo wa nyuklia na kiulinzi wa Iran, sio tu kwamba haikufikia malengo yake, bali pia iliimarisha mshikamano wa ndani wa Iran na kuongeza nguvu ya kitaifa ya kuzuia hujuma ya adui. Araghchi amesema kuwa Iran sasa ina "maandalizi mapana na ya kina" ikilinganishwa na kipindi hicho, na kwamba chokochoko zozote mpya za Marekani zitakabiliwa na jibu kali zaidi.
Jambo la pili ni hali ya ndani na kieneo. Wakati Marekani imezama katika mvutano wa kisiasa na maandamano ya ndani, kuingia katika mgogoro mwingine wa kigeni kunaweza kuwa na matokeo yasiyotabirika kwa Washington. Akiashiria hali hii, Araghchi ameonya kwamba Trump hapaswi kufikiria kuwa hatua ndogo ya kijeshi inaweza kugeuza kirahisi maoni ya umma ya Marekani au kumletea mafanikio ya haraka. Uzoefu wa vita vya siku 12 ulionyesha kwamba Iran ina uwezo wa kukabiliana na matabaka meingi na ya muda mrefu ya maadui, na kwamba mzozo wowote unaweza kugeuka kuwa mgogoro mkubwa wa kikanda.
Sababu ya tatu ni ujumbe wa kuzuia hujuma ya Marekani na washirika wake. Katika maneno yake, Araghchi amesisitiza kwamba Iran "haitaki vita, lakini iko tayari kwa ajili ya vita" na utayari huu ni imara zaidi sasa kuliko ilivyokuwa huko nyuma. Ujumbe huu umetolewa ili kuzuia mahesabu mabaya huko Washington, mahesabu ambayo kwa hakika hayakuwa sahihi pia katika vita vya siku 12. Kwa kuonyesha uwezo wake wa makombora, ndege zisizo na rubani na kiulinzi katika vita hivyo, Iran ilithibitisha kuwa shambulio lolote dogo linaweza kukabiliwa na jibu pana na kali zaidi ya matarajio.
Jambo la nne ni kujaribu kudumisha njia ya diplomasia sambamba na juhudi za kuzuia hujuma. Licha ya maonyo ya wazi, Araghchi ametangaza mara kwa mara kwamba Iran itaendelea kuweka wazi mlango wa mazungumzo, lakini kwa sharti kwamba Marekani iache vitisho na mashinikizo. Mchanganyiko huu wa "uzuiaji mgumu" na "utatuzi wa kidiplomasia" ni sehemu ya mkakati mkuu wa Iran wa kudhibiti mgogoro na Marekani.
Kwa jumla, onyo la Araghchi kwa Trump kuhusu kutorudia uzoefu uliofeli wa vita vya siku 12 linatokana na uchambuzi wa kina wa uwezo wa kiulinzi wa Iran, hali ya ndani ya Marekani, matokeo ya kieneo ya mzozo wowote ule, na haja ya kuepukwa mahesabu mabaya huko Washington. Ujumbe huu wa wazi unasema kwamba njia ya mashinikizo na vitisho sio tu haina matokeo kwa Marekani, bali pia inaweza kuisababishia hasara kubwa. Hii ni katika hali ambayo njia ya mazungumzo bado iko wazi ikiwa itaambatana na siasa za pande mbili kuheshimiana.