Palestina: Idadi ya watoto wanaozaliwa wakiwa vilema inaongezeka
-
Palestina: Idadi ya watoto wanaozaliwa wakiwa vilema inaongezeka
Mkuu wa idara ya habari ya Wizara ya Afya ya Palestina huko Gaza ametangaza kuwa, idadi ya watoto wanaozaliwa wakiwa vilema inazidi kuongezeka katika Ukanda huo unaokabiliwa na hali mbaya ya kibinadamu.
Zaher al-Wahidi ameeleza kuwa, mwaka uliopita 2025, idadi ya watoto wanaozaliwa mapema na kuzaliwa kwa watoto wenye kasoro za viungo na uzito usio wa kawaida katika Ukanda wa Gaza iliongezeka kwa kiwango cha kutisha; hali ambayo anasema ni matokeo ya moja kwa moja ya vita vya utawala haramu wa Israel na matokeo yake ya kibinadamu.
Al-Wahidi ameongeza kuwa, mnamo 2025, takriban watoto 49,180 walizaliwa, wakiwemo watoto 4,900 wenye uzito usio wa kawaida na watoto 4,000 waliozaliwa kabla ya wakati. Aliongeza: "Tumerekodi kuzaliwa kwa watoto 315 wenye matatizo ya kuzaliwa nayo, ikiwa ni pamoja na kasoro katika viungo kama vile moyo na kibofu cha mkojo, miongoni mwa wengine."
Wakati huo huo, Mkurugenzi wa kitengo cha takwimu cha Wizara ya Afya ya Palestina katika Ukanda wa Gaza amesema, tangu kuanza vita vya Gaza Oktoba 7, 2023 hadi mwishoni mwa mwaka 2024, kesi 4,500 za kukatwa miguu sehemu ya juu au ya chini zilirekodiwa ikiwa ni matokeo ya mashambulizi ya anga na ardhini yanayoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni.
Takwimu za watu kukatwa viungo huko Gaza zinaonyesha ukubwa wa maafa ambayo raia wa Palestina wanakabiliana nayo, na kutokana na kutowezekana kukusanya takwimu sahihi kutokana na kuendelea vita hivyo, madaktari na maafisa wa serikali wanatabiri kwamba idadi ya kesi za kukatwa viungo, haswa miongoni mwa watoto, ni mara kadhaa ya takwimu zilizotangazwa.