Rached Ghannouchi Kiongozi wa Ennahda Tunisia atimiza siku 1,000 jela
-
Rached Ghannouchi
Rached Ghannouchi kiongozi wa chama cha Kiislamu chenye ushawishi mkubwa nchini Tunisia cha al-Nahdha na Spika wa zamani wa bunge la nchi hiyo jana Jumapili alitimiza siku 1,000 akiwa kifungoni jela. Ghannouchi ametaja kifungo kinachomkabili kuwa ni " wakati wa mahesabu ya kisiasa."
Ghannouchi ametuma ujumbe katika ukurasa rasmi wa mtandao wa Facebook wa harakati ya Al-Nahdha akiwa katika gereza la Mornaguia kwamba kifungo chake kinaakisi kiwango ambacho kanuni za kidemokrasia na uraia sawa kinavyotekelezwa nchini Tunisia.
Kwa maoni yake amesisitiza kuwa suala la kutengwa kisiasa na ubabe bado vina mfungamano wa karibu. Katika ujumbe wake huo, kiongozi huyo wa harakati ya al-Nahdha amesisitiza kuwa kihistoria harakati hiyo imekuwa ikiunga mkono mfumo wa demokrasia ya vyama vingi na haki ya pande zote kushiriki wazi shughuli mbalimbali za kisiasa , kijamii n.k bila kujali tofauti za kiitikadi.
Katika ujumbe wake huko aliotuma jana baada ya kutimiza siku 1,000 gerezani, Spika huyo wa zamani wa bunge la Tunisia amevitolea wito vyama vya siasa kudumisha umoja na mshikamano nchini humo.
Amesema, Watunisia wanapasa kujiepusha na mifarakano na migawanyiko; na badala yakecwafanye kazi kwa pamoja ili kudumisha amani na utulivu nchini humo.
Ghannouchi,mwenye umri wa miaka 84, ameshikiliwa tangu Aprili 2023; na kwa sasa anatumikia vifungo kadhaa jela nchini Tunisia baada ya kuhukumiwa ikiwa ni pamoja na hukumu ya miaka 22 iliyothibitishwa hivi karibuni na mahakama ya rufaa. Mamlaka za Tunisia zinasema mashtaka ni ya jinai yanayohusiana na usalama wa taifa, lakini wapinzani wanasema ni kampeni ya kisiasa dhidi ya wapinzani wa Rais Kais Saeid.