Wahamiaji 50 wahofiwa kufa maji katika ajali ya boti pwani ya Tunisia
Serikali ya Tunisia imesema kuwa, takriban wahamiaji 50 aghalabu yao kutoka Kusini mwa Jangwa la Sahara barani Afrika wanahofiwa kufariki dunia baada ya mashua yao kupinduka katika pwani ya Tunisia.
"Mhamiaji mmoja ameokolewa na wengine 50 wanahofiwa kufa maji baada ya boti kuzama katika Bahari ya Mediterania," maafisa wa serikali ya Tunisia walisema jana Jumapili.
Mwanamume huyo alisalia majini kwa saa 24 baada ya ajali, na anasema anaamini kwamba wasafari wenzake wote waliokuwa kwenye chombo hicho wamefariki dunia, hayo ni kwa mujibu wa kundi la 'Alarm Phone' ambalo linapokea simu za dharura za wahamiaji.
Kundi hilo limesema, boti hiyo ilikuwa imetoka Tunisia, mahali pa kawaida pa kuondokea wahamiaji wanaohatarisha maisha yao ili kwenda Ulaya.
Mwanamume huyo aliokolewa na meli ya biashara nje ya pwani ya Tunisia na kupelekwa Malta kwa ajili ya matibabu, jeshi la Malta limesema.
Tukio la sasa linaangazia hatari zinazowakabili wahamiaji na mashinikizo yanayoongezeka kwa nchi za Kaskazini mwa Afrika ili kudhibiti njia zisizo za kawaida za wahamiaji.
Kila mwaka, maelfu ya watu wanajaribu kutumia njia hatari ya kuvuka bahari ya Mediterrania, ambayo inaonekana kujaa boti chakavu, huku kukiwa na hatari zilizochangiwa na hali mbaya ya hewa.