Vyama vya Tunisia vyamjia juu Trump kwa kukiuka sheria za kimataifa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i135240-vyama_vya_tunisia_vyamjia_juu_trump_kwa_kukiuka_sheria_za_kimataifa
Vyama vya kisiasa na harakati za kijamii na kiraia nchini Tunisia zimetangaza kupinga vikali ajenda ya sera ya kigeni ya Rais wa Marekani Donald Trump, hasa uingiliaji wake wa masuala ya ndani ya Venezuela na ushupaliaji wake wa kutaka kuidhibiti Greenland.
(last modified 2026-01-08T06:09:31+00:00 )
Jan 08, 2026 06:09 UTC
  • Vyama vya Tunisia vyamjia juu Trump kwa kukiuka sheria za kimataifa

Vyama vya kisiasa na harakati za kijamii na kiraia nchini Tunisia zimetangaza kupinga vikali ajenda ya sera ya kigeni ya Rais wa Marekani Donald Trump, hasa uingiliaji wake wa masuala ya ndani ya Venezuela na ushupaliaji wake wa kutaka kuidhibiti Greenland.

Wadau wa kisiasa nchini Tunisia wameuelezea misimamo hiyo ya Trump kuwa ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na muendelezo wa sera ya muda mrefu ya kibeberu ya Marekani duniani.

Hali kadhalika vyama hivyo vys kisiasa na kijamii nchini Tunisia vimelaani vikali kitendo cha Washington cha kumteka nyara Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro.

Vimesema hatua ya Marekani ya kuishambulia Venezuela na kumteka nyara Maduro inachukuliwa kuwa shambulio kubwa dhidi ya uhuru na mamlaka ya kujitawala nchi nyingine.

Matamshi ya Trump ya kutangaza azma yake na kuitwaa Greenland yameibua hofu nchini Denmark na katika nchi za Ulaya, hasa kutokana na uvamizi wa kijeshi wa hivi karibuni wa Washington dhidi ya Venezuela, ikiwa ni pamoja na kutekwa nyara kwa Rais Maduro na mkewe, Cilia Flores. Katika kujibu bwabwaja za Trump, viongozi wa Ufaransa, Ujerumani, Uingereza na nchi nyingine kadhaa waliungana na Waziri Mkuu wa Denmark, Mette Frederiksen, Jumanne kuitaka Washington kuheshimu uhuru wa Denmark na sheria za kimataifa.

Aidha Josep Borrell, mwanadiplomasia mkuu wa zamani wa Umoja wa Ulaya (EU) amesema, kambi hiyo inapaswa iache kuichukulia Marekani kama mshirika wake mkuu, huku Washington na Brussels zikiwa zinazozana hivi sasa kuhusu sera za kidijitali na udhibiti wa eneo la Greenland.

Kadhalika Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa operesheni ya kijeshi ya Marekani nchini Venezuela ilikuwa ukiukaji wa sheria za kimataifa na Hati ya Umoja wa Mataifa.