Watu 53 wahofiwa kufa maji baada ya boti kuzama pwani ya Libya
Watu wasiopungua 53 wakiwemo watoto wawili wadogo wameripotiwa kwamba, ama wamekufa maji au kutoweka, baada ya boti dhaifu ya plastiki iliyokuwa imebeba makumi ya wahajiri kuzama karibu na pwani ya Libya.
Katika taarifa iliyotolewa leo Jumatatu, Shirika la Kimataifa la Uhamiaji limesema boti hiyo ilipinduka kaskazini mwa mji wa pwani wa Zuwara, kaskazini magharibi mwa Libya, mnamo Februari 6.
Hakuna maelezo ya kina yaliyotolewa kuhusu uraia wa wahajiri hao, ingawaje katika wiki za hivi karibuni, matukio kama hayo yamekuwa yakitokea mara kwa mara katika pwani ya Libya, yakiwahusisha wahamiaji wa Kiafrika wasio na hati za kusafiria wakijaribu kuvuka Bahari ya Mediterania kuelekea Ulaya kwa tamaa chapwa za kupata maisha bora.
Sehemu kubwa ya wahamiaji hao haramu huishia kufa maji baharini au kuingia kwenye mikono ya magenge hatari ya magendo ya binadamu na kupigwa mnada masokoni kama bidhaa zisizo na thamani.
Shirika la Kupambana na Uhamiaji Haramu la Libya limezitaja "boti za mauti" kuwa ni tishio kubwa kwa maisha ya binadamu, hasa wakati hali ya hewa inapokuwa mbaya na mawimbi ya maji yapokuwa makubwa baharini.
Libya kwa muda mrefu imekuwa kitovu cha usafiri kwa wahamiaji 'haram' kutokana na nchi hiyo kuwa katika eneo muhimu la kijiografia na kuwa karibu kwake na bara Ulaya.
Tangu ulipoangushwa utawala wa kiongozi wa zamani Kanali Muammar Gaddafi mwaka 2011, Libya imeshindwa kuwa na utulivu na hakuna serikali yenye nguvu nchini humo, suala ambalo limeifanya nchi hiyo kuvamiwa na mitandao ya magendo na kufanya kazi zao kwa uhuru.