Umoja wa Mataifa waonya kuhusu hali mbaya ya kibinadamu Sudan
-
Umoja wa Mataifa waonya kuhusu hali mbaya ya kibinadamu Sudan
Umoja wa Mataifa umeonya kuhusu hali mbaya ya kibinadamu nchini Sudan huku vita vya wenyewe kwa wenyewe vikiendelea nchini humo.
Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu ameonya kwamba vita vya Sudan vinaipeleka nchi hiyo kwenye uharibifu. Alitaja mashambulizi ya mara kwa mara ya Vikosi vya RSF dhidi ya miundombinu ya kiraia ya Sudan, ikiwa ni pamoja na Bwawa la Merwi, ambalo hutoa asilimia 70 ya umeme nchini humo.
Katika upande mwingine idadi ya wakimbizi inazidi kuongezeka huku mauaji yakiripotiwa katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.
Baada ya zaidi ya miaka miwili ya mapigano makali kati ya jeshi la taifa na wanamgambo wa Rapid Support Forces (RSF), serikali ya Sudan imerejea rasmi mjini Khartoum, hatua ambayo Waziri Mkuu Kamel Idris aliitaja kuwa “mgeuko muhimu katika safari ya taifa.”
Mnamo Mei 21 mwaka jana, jeshi la Sudan lilitangaza kurejesha udhibiti kamili wa Khartoum, likisema mji mkuu uko huru kutoka RSF baada ya mapigano katika eneo la Salha kusini mwa jiji. Mwezi Julai mwaka jana, Mwenyekiti wa Baraza la Mpito la Uongozi, Abdel Fattah al‑Burhan, aliunda kamati ya kitaifa kuandaa mazingira ya kurejea kwa taasisi za shirikisho na wakazi wa Khartoum. Kwa sasa, RSF inadhibiti majimbo yote matano ya Darfur isipokuwa sehemu za kaskazini mwa Darfur Kaskazini, huku jeshi likidhibiti maeneo mengi ya majimbo 13 yaliyosalia, ikiwemo Khartoum.
Mgogoro wa kibinadamu nchini Sudan umeendelea kuwa mbaya zaidi tangu Aprili 2023, wakati vita vilipozuka kutokana na mvutano kuhusu kuunganisha vyombo vya ulinzi. Mapigano hayo yamesababisha vifo vya makumi ya maelfu na mamilioni kuyahama makazi yao, na hivyo kuifanya Sudan kuwa moja ya maeneo yenye mgogoro mkubwa zaidi barani Afrika.