Baraza la Katiba CAR lamtangaza Rais Faustin-Archange Touadéra kuwa alishinda uchaguzi
-
Je, Trump anajaribu kufidia udhalilishaji wa kihistoria iliofanyiwa Marekani 2016 na Iran?
Baraza la Katiba nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, limetangaza mnamo Januari 19, 2026, kuchaguliwa tena Rais Faustin-Archange Touadéra kwa muhula wa tatu.
Baraza la Katiba limeamua kuwa haikubaliki kwa misingi ya utaratibu rufaa ya kufuta uchaguzi huo iliyowasilishwa na mpinzani wake mkuu, Anicet-Georges Dologuélé.
Kulingana na matokeo ya mwisho ya uchaguzi wa Desemba 28, Faustin-Archange Touadéra alipata 77.9% ya kura dhidi ya 13.5% ya kura alizopata mgombea wa upinzani, ambaye alilaani udanganyifu mara kadhaa. Idadi ya wapiga kura ilirekebishwa hadi 64.42%.
Mapema mwezi Januari Mamlaka ya Uchaguzi nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati ilitangaza kwamba Rais Faustin-Archange Touadéra alichaguliwa tena kwa asilimia 76.15 ya kura. Sehemu ya upinzani ilisusia uchaguzi huo.
Faustin-Archange Touadéra ambaye alichaguliwa mwaka wa 2016 na kisha kuchaguliwa tena mwaka wa 2020 katika uchaguzi uliojaa tuhuma za udanganyifu, anakosolewa kwa kupitisha Katiba mpya mwaka wa 2023 iliyomruhusu kusalia madarakani.
Kiongozi wa upinzani Anicet-Georges Dologuélé analaani kile anachokiita udanganyifu mkubwa, uliopangwa na serikali na unaofanywa na Tume Huru ya Uchaguzi.
Anicet-Georges Dologuelé anaishutumu serikali kwa kuweka mifumo ya kuiba matokeo ya uchaguzi, kwa usaidizi wa Mamlaka ya Kitaifa ya Uchaguzi. Kiongozi huyo wa upinzani anadai ushindi kulingana na data zilizokusanywa katika vituo mbalimbali vya kupigia kura na timu yake na waangalizi wa kuaminika.
Mamlaka ya Uchaguzi katika Jamhuri ya Afrika ya Kati imetangazia umma na jumuiya ya kimataifa kuhusu uwazi wa mchakato unaoendelea.