Makanisa ya al-Quds yaonya kuwa ‘Uzayuni wa Kikristo’ unahatarisha Ukristo
Viongozi wakuu wa Kikristo katika mji wa Palestina wa al-Quds (Jerusalem) unaokaliwa kwa mabavu na Israel, wameonya kuwa “Uzayuni wa Kikristo” pamoja na ajenda za nje zinavunja umoja wa Wakristo katika Ardhi Takatifu na kudhoofisha mamlaka yao ya kiroho na kijamii.
Viongozi hao walionya dhidi ya vitendo vya baadhi ya watu katika maeneo yanayokaliwa na Israel wanaosukuma itikadi hatari kama “Uzayuni wa Kikristo,” wakisema juhudi hizo “zinapotosha umma, zinachanganya fikra, na kuathiri umoja wa kundi letu la waumini.”
Mapatriaki hao walisema pia kuwa wana “wasiwasi mkubwa” kwamba wanaosukuma ajenda hizo “wamekuwa wakipokelewa katika ngazi za juu, ndani ya eneo na hata kimataifa.”
Aidha, waliitaja aina hiyo ya ushirikiano kama kuingilia maisha ya ndani ya makanisa na kupuuza mamlaka ya kichungaji ambayo imekabidhiwa uongozi wa makanisa ya al-Quds.
Kauli hiyo imekuja wakati ambapo mkondo wenye nguvu wa Ukristo wa kiinjili pamoja na wafuasi wa mrengo wa kulia wanaomuunga mkono Rais Donald Trump nchini Marekani unaendelea kuathiri mwelekeo wa kisiasa na kifedha wa uungaji mkono kwa Israel, jambo ambalo limezidi kuwatia wasiwasi viongozi wa makanisa katika al-Quds inayokaliwa kwa mabavu.
Onyo hilo pia linakuja wakati ambapo kuna wasiwasi unaoongezeka miongoni mwa Wakristo wa Kipalestina kwamba sera za Israel zinaharakisha kuporomoka kwa moja ya jamii za Kikristo za zamani zaidi duniani.
Ripoti ya hivi karibuni iliyotolewa na kamati ya vyombo vya juu vya makanisa ya Kipalestina imesisitiza haja ya dharura ya kulinda jumuiya za Kikristo na maeneo ya ibada katika Ukingo wa Magharibi, ambako mashambulizi ya walowezi yamekuwa yakilenga kwa kiwango kinachoongezeka makanisa, watu, na mali zao.
Mnamo Jumatano, ripoti hiyo ililaani vizuizi vinavyowekwa na Israel vinavyowazuia walimu kutoka Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu kufika katika shule zilizoko Mashariki mwa al-Quds, ikionya kuwa elimu ya Kikristo iko chini ya shambulio la moja kwa moja.
Kamati hiyo ilionya kuwa kulengwa kwa shule za Kikristo ni sehemu ya sera pana ya Israel inayolenga kudhoofisha elimu ya Kipalestina na kupunguza uwepo wa Wakristo wa Kipalestina katika mji wa al-Quds unaokaliwa kwa mabavu. Tayari utawala haramu wa Isarel unatekeleza sera za kuwatimua Waislamu katika mji huo na kuharibu turathi za Kiislamu hasa Msikiti wa Al Aqsa. Lengo kuu la utawala dhalimu wa Israel ni kuuyahidisha kikamlifu mji huo.