Dakta Zarif: Tishio pekee kwa utawala wa Israel ni amani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i128474
Aliyekuwa Makamu wa Rais wa Masuala ya Kistratejia wa Iran, Mohammad-Javad Zarif amesema kuwa, tishio pekee lililopo kwa utawala wa Kizayuni wa Israel ni amani.
(last modified 2025-07-18T14:12:38+00:00 )
Jul 18, 2025 14:02 UTC
  • Dakta Zarif: Tishio pekee kwa utawala wa Israel ni amani

Aliyekuwa Makamu wa Rais wa Masuala ya Kistratejia wa Iran, Mohammad-Javad Zarif amesema kuwa, tishio pekee lililopo kwa utawala wa Kizayuni wa Israel ni amani.

Dakta Zarif ameorodhesha msururu wa uhalifu wa Israel, ikiwa ni pamoja na uvamizi wa Syria, uvamizi wa Lebanon, vita dhidi ya Iran, mauaji ya halaiki huko Gaza, na shambulio la mabomu huko Yemen kama mifano hai ya kutofadhilisha amani utawala huo haramu.

Aidha Zarif, ambaye amewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema mifano mingine ya wazi kuwa Israel haipendi amani ni upinzani wake kwa Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA), Mkataba wa Kuzuia Uzalishaji na Uenezi wa Silaha za Nyuklia (NPT), Mkataba wa Silaha za Kemikali, na makubaliano yanayohusiana na silaha za maangamizi makubwa, pamoja na kuzuia kwake juhudi za amani-hata zile zilizopendekezwa na Marekani na Umoja wa Ulaya.

"Kwa hivyo: Vita, ugaidi, hujuma, usaliti ... zinaonyesha kwamba 'tishio pekee lililopo' kwa Israel ni amani," Zarif ameandika kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa X leo Ijumaa.

Huko nyuma, Dakta Zarif alisema Jamhuri ya Kiislamu si tishio la usalama kwa nchi yoyote ile duniani, akisisitiza kwamba kama Tehran ingelikusudia kutengeneza silaha za nyuklia, ingelikuwa imefanya hivyo zamani.

Alisisitiza kuwa, "Iran sio tishio la usalama. Baadhi wanajaribu kuiarifisha Iran kama tishio la usalama na kutumia chuki dhidi ya Iran (Iranophobia) na chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia) kuhalalisha matendo yao dhidi ya watu wasio na hatia, ikiwa ni pamoja na Gaza. Hata hivyo, madai haya hayana msingi wowoye.”