6 wauawa, 100 watekwa katika shambulio la majambazi Zamfara, Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i128488-6_wauawa_100_watekwa_katika_shambulio_la_majambazi_zamfara_nigeria
Watu wenye silaha wameripotiwa kuwauwa watu wasiopungua sita na kuwateka nyara wengine zaidi ya 100, wakiwemo wanawake na watoto, katika shambulio dhidi ya watu wa jamii ya Kairu katika jimbo la Zamfara, kaskazini magharibi mwa Nigeria.
(last modified 2025-10-16T03:06:03+00:00 )
Jul 18, 2025 16:35 UTC
  • 6 wauawa, 100 watekwa katika shambulio la majambazi Zamfara, Nigeria

Watu wenye silaha wameripotiwa kuwauwa watu wasiopungua sita na kuwateka nyara wengine zaidi ya 100, wakiwemo wanawake na watoto, katika shambulio dhidi ya watu wa jamii ya Kairu katika jimbo la Zamfara, kaskazini magharibi mwa Nigeria.

"Majambazi hao walivamia eneo la Kairu jana Ijumaa, na kufyatua risasi kiholela," Abubakar Isa, mkazi ambaye mkewe alitekwa nyara, ameliambia shirika la habari la Reuters kwa njia ya simu.

Naye Hamisu Faru, mbunge wa eneo hilo, amethibitisha habari za kujiri shambulio hilo katika mahojiano na Reuters, akisema washambuliaji waliwateka "watu wasiopungua 100, wakiwemo wanawake na watoto."

Zamfara ni kitovu cha mashambulizi ya magenge ya watu wenye silaha nzito, wanaojulikana na wakazi kama majambazi, mashambulizi ambayo yamesababisha uharibifu katika kaskazini magharibi mwa Nigeria katika miaka ya hivi karibuni.

Aidha magenge hayo huwateka nyara maelfu ya watu, na kuua mamia, wimbi la uhalifu ambalo limevuruga usafiri kwa njia ya barabara, na pia shughuli za kilimo mashambani katika baadhi ya maeneo.

Shambulio la Zamfara limejiri siku chache baada ya watu wasiopungua 27 kuuawa katika shambulio jingine lililofanywa na watu wenye silaha kaskazini kati mwa jimbo la Nigeria la Plateau, katika machafuko ya hivi karibuni yaliyolikumba eneo hilo ambalo halina usalama wa kutosha.

Katika mwezi Aprili pekee, mashambulizi yaliyofanywa kote katika jimbo la Plateau na jimbo la jirani la Benue yalisababisha vifo vya watu zaidi ya 150.

Katika miaka kadhaa ya hivi karibuni, mashambulizi ya watu wenye silaha yameongezeka vijijini kaskazini magharibi na katikati mwa Nigeria, taifa ambalo linasumbuliwa pia na hujuma za magenge ya kigaidi kama Boko Haram na AQIM.