UNESCO yailaani Israel kwa mauaji ya wanahabari wa Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i128470-unesco_yailaani_israel_kwa_mauaji_ya_wanahabari_wa_iran
Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) limelaani mauaji ya wafanyakazi wawili wa vyombo vya habari wa Iran wakati wa mashambulizi ya anga ya Israel kwenye makao makuu ya Shirika la Utangazaji la Iran, IRIB mjini Tehran mwezi uliopita.
(last modified 2025-07-18T13:47:19+00:00 )
Jul 18, 2025 13:28 UTC
  • UNESCO yailaani Israel kwa mauaji ya wanahabari wa Iran

Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) limelaani mauaji ya wafanyakazi wawili wa vyombo vya habari wa Iran wakati wa mashambulizi ya anga ya Israel kwenye makao makuu ya Shirika la Utangazaji la Iran, IRIB mjini Tehran mwezi uliopita.

Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO Audrey Azoulay ametoa wito wa uchunguzi wa kina na wa uwazi juu ya shambulio hilo. Amesisitiza kuwa, miundombinu ya vyombo vya habari ya kila nchi inalindwa chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu, kwani imeainishwa kama taasisi ya kiraia.

Azoulay ameashiria Azimio nambari 2222 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambalo linaamuru ulinzi wa wafanyikazi wa vyombo vya habari wakati wa migogoro ya silaha.

Shambulio hilo la kinyama la Israel lilipelekea kuuawa shahidi Nima Rajabpour, aliyekuwa Mhariri Mkuu wa kituo cha habari cha IRIB, na Masoumeh Azimi, msimamizi wa kituo hicho. 

Shambulio hilo pia lilijeruhi wanahabari wengine kadhaa. Tarehe 16 Juni, utawala wa Israel ulifanya kitendo cha uchokozi kwa kulenga jengo la Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (IRIB) mjini Tehran.

Shambulio hilo lilihusisha angalau mabomu manne, na kushambulia kituo kikuu cha idara ya habari ya IRIB wakati matangazo ya moja kwa moja yakiendelea.

Upeperushaji wa matangazo ya moja kwa moja ulikatizwa kwa muda kabla ya Hassan Abedini, Mkurugenzi wa Habari wa IRIB na naibu wa masuala ya kisiasa, kwenda hewani kulaani shambulio hilo.