AU yamteua Rais wa Burundi kuwa mjumbe wake maalum eneo la Sahel
Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), Joao Lourenco ametangaza kumteua Evariste Ndayishimiye, Rais wa Burundi, kuwa mjumbe wake maalum katika eneo la Sahel.
Ndayishimiye ataongoza usaidizi wa ngazi ya juu wa kidiplomasia wa AU na juhudi shirikishi zinazolenga kutatua changamoto za kiusalama na kibinadamu katika eneo la Sahel, AU imetangaza katika taarifa yake ya jana Alkhamisi.
Jukumu la mjumbe maalum linahusu kuimarisha mashirikiano na mamlaka za serikali, viongozi wa mashirika yasiyo ya serikali, watendaji na mashirika ya kikanda, mashirika ya kiraia na washikadau wote husika ili kukuza mazungumzo, kujenga makubaliano, na kukuza mikakati ya kina kuelekea amani na utulivu wa kudumu ndani ya eneo la Sahel.
Ndayishimiye analeta tajiriba kubwa sana ya uzoefu wa kisiasa, na sifa kamilifu za kujitolea kwa uthabiti kwa uanamajimui wa Afrika (Pan-Africanism), ushirikiano wa kikanda na utangamano, taarifa hiyo imebainisha.
Lourenco, ambaye pia Rais wa Angola, ameonyesha imani katika uwezo wa Rais wa Burundi kuendeleza dira ya umoja huo kupitia uongozi wake imara na uelewa wa kina wa mienendo tata ya bara hilo.
Haya yanajiri siku chache baada ya Rais wa mpito wa Burkina Faso, Kapteni Ibrahim Traoré, kuzishutumu nchi za kigeni kwa kujaribu kuhujumu Muungano wa Mataifa ya Sahel (AES) kwa kuwachochea wanachama kusalitiana.
Traoré alionya kuwa, juhudi za Magharibi za kuichafua Sahel zinaendeshwa na tamaa ya rasilimali lukuki za asili ambazo bado hazijagunduliwa wala kutumika ipasavyo katika eneo hilo.