Amnesty: Rais wa Burundi anakanyaga haki za binadamu
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limesema katika ripoti yake mpya kwamba, Burundi imeshuhudia vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu katika kipindi cha miaka minne ya utawala wa Rais wa nchi hiyo, Evariste Ndayishimiye.
Ripoti hiyo imebainisha kuwa, kipindi hicho kimetawaliwa na vitendo vya ukiukaji wa haki vikiwemo unyanyasaji, watu kukamatwa kiholela, mashtaka yasiyo ya haki pamoja na vitisho.
Taarifa ya Amnesty International imebainisha kuwa, miongoni mwa waliokabiliwa zaidi na ukandamizaji huo wa haki ni watetezi wa haki za binadamu, wanaharakati, waandishi wa habari na wanachama wa vyama vya upinzani.
Akizungumza wakati wa kutoa ripoti hiyo, Mkurugenzi wa shirika hilo katika kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Tigere Chagutah, ameeleza kuwa, wimbi hilo la dhulma na ukandamizaji linaloendelea kushuhudiwa Burundi, limefifisha matumaini ya mabadiliko ya maana kwa asasi za kiraia nchini humo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, baada ya maandamano makubwa ya mwaka 2015 na jaribio la mapinduzi ya kijeshi, serikali ya rais wa zamani wa Burundi Pierre Nkurunziza, ilichukua hatua kali zilizosababisha moja ya asasi maarufu za kiraia nchini humo kushindwa kuendelea na shughuli zake kama hapo awali.
Disemba mwaka jana, Rais wa Burundi alitoa mwito wa kupigwa mawe hadharani watu wanaojihusisha na ushoga na maingiliano ya watu wenye jinsia moja, mwito uliokosolewa vikali na madola ya Magharibi na taasisi zake. Kabla ya hapo, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu ilisema imeshtushwa na madai ya kuaminika ya unyanyasaji, kuteswa, kunyongwa bila haki na watu kutoweshwa nchini Burundi tangu mzozo wa kisiasa wa mwaka 2015.