Jumanne tarehe Mosi Julai, 2025
Leo ni Jumanne tarehe 05 Muharram 1447 Hijria sawa na Julai Mosi mwaka 2025.
Siku kama ya leo mika 1386 iliyopita, baada ya Ubaidullah bin Ziyad kutuma kikosi cha askari wengine 1000 kuelekea Karbala kwa ajili ya kupigana vita na mjukuu wa Mtume Muhammad (saw), Imam Hussein (as), alimpa jukumu bwana mmoja aliyejulikana kwa jina la Zahr ibn Qais aliyekuwa na wapanda farasi 500 wasimame katika daraja la Sadah katika mji wa Kufa na awazuie watu wanaotaka kutoka katika mji huo na kwenda kuungana na Imam Hussein (as).
Mtu aliyejuliana kwa jina la Ammar au A'mir bin Abi Salamah aliyekuwa ameazimia kwenda kuungana na Imam Hussein alipambana na Zahr na jeshi lake na kufanikiwa kutoka nje ya Kufa. Hakuna mtu aliyethubutu kumfuata.
A'mir alifanikiwa kufika Karbala na kuungana na Imam Hussein (as), na akiwa huko alifanikiwa kupata daraja kubwa ya kuuliwa shahidi akiwa pamoja na mjukuu wa Mtume.
A'mir bin Abi Salamah alikuwa mmoja kati ya masahaba wa Mtume Muhammad (saw) na watu wa karibu kwa Imam Amirul-Muuminin Ali bin Abi Twalib (as) na alishiriki katika vita vingi akiwa pamoja na mtukufu huyo.

Siku kama ya leo miaka 237 iliyopita alizaliwa Jean Victor Poncelet mwasisi wa uchambuzi wa maumbo.
Victor Poncelet aliyekuwa mtaalamu maarufu wa hisabati wa Ufaransa, alitambulika kuwa mwasisi wa uchambuzi wa maumbo. Poncelet alikuwa mmoja wa maafisa wa jeshi la Napolione na alitekwa nyara na Warusi wakati jeshi la Ufaransa lilipokuwa likirejea nyuma kutoka Urusi ya zamani.
Hata hivyo katika kipindi cha kutekwa alijiendeleza kielimu na kukamisha elimu yake ya uhandisi. Jean Victor Poncelet alifariki dunia tarehe 22 Disemba 1867.

Siku kama ya leo miaka 158 iliyopita, nchi ya Canada ilijitangazia uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza.
Canada iligunduliwa mwishoni mwa karne ya 15 Miladia na kuanzia wakati huo kwa zaidi ya karne mbili, Uingereza na Ufaransa zilikuwa zikishindana katika ardhi ya nchi hiyo kwa lengo la kupanua udhibiti wao. Ushindani huo ulipelekea kujiri vita kati ya mataifa hayo ya kikoloni ambapo mwaka 1689 vita hivyo vilidumu kwa karibu miaka 75 vilimalizika kwa kushindwa Ufaransa.
Kuanzia mwanzoni mwa karne ya 19 taratibu zilianza harakati za kupigania uhuru wa Canada ambazo zilizaa matunda mwaka 1867 katika siku kama ya leo.

Miaka 65 iliyopita katika siku kama ya leo, sehemu mbili za Somalia ya Uingereza na ya Italia ziliungana na kuunda nchi moja ya Somalia yenye kujitawala.
Karne kadhaa nyuma, Somalia iliwahi kujitawala kwa kipindi kifupi. Mwaka 1884 Uingereza iliiweka katika himaya yake sehemu ya ardhi ya nchi hiyo. Miaka mitano baadaye Italia nayo ikakoloni baadhi ya sehemu za Somalia.
Harakati za mapambano za Muhammad Abdullah Hassan dhidi ya Waingereza kuanzia mwaka 1901 hadi 1920 hazikuzaa matunda. Mwaka 1950 Umoja wa Mataifa uliitaka Italia iandae mazingira ya kujitawala na kuwa huru nchi ya Somalia.

Katika siku kama ya leo miaka 63 iliyopita, nchi ndogo ya Burundi ilijitangazia uhuru wake.
Kuanzia mwaka 1899 hadi 1917 Burundi pamoja na Rwanda ilikuwa sehemu ya makoloni ya Mjerumani huko Afrika Mashariki. Baada ya Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia na kushindwa Ujerumani katika vita hivyo, Umoja wa Mataifa uliikabidhi Ubelgiji ardhi ya Burundi. Mwaka 1962 Burundi ilipata uhuru ikiwa na mfumo wa utawala wa kifalme.
Hata hivyo miaka minne baadaye wapigania jamhuri walimuondoa madarakani mfalme na kuanzisha mfumo wa serikali ya jamhuri.

Na siku kama ya leo miaka 63 iliyopita, Rwanda ilipata uhuru.
Rwanda ina historia inayofanana na jirani yake wa kusini yaani Burundi ambapo kabla ya nchi hizo kujitangazia uhuru zilikuwa zikikoloniwa na Ubelgiji. Baada ya mapambano mtawalia ya wapigania uhuru wa Rwanda, hatimaye mnamo mwaka 1962, nchi hiyo ilipata uhuru na kabila kubwa la Wahutu likashika hatamu za uongozi wa nchi.
Mwaka 1973, Meja-Jenerali Juvenal Habyarimana alichukua madarakani baada ya kufanya mapinduzi yasiyo na umwagaji damu. Hata hivyo mwaka 1994 kulitokea mauaji ya kimbari ambapo zaidi ya watu laki 8 waliuawa wengi wao wakiwa ni wa kabila la Tutsi.
