Jul 29, 2026 02:38 UTC
  • Leo katika Historia
    Leo katika Historia

Leo ni Jumatano tarehe 14 Mfunguo Tano Safar 1448 Hijria mwafaka na tarehe 29 Julai 2026.

Katika siku kama ya leo miaka 816 iliyopita sawa na tarehe 14 Safar mwaka 632 Hijria alifariki dunia Abul Mahasin Bahauddin mashuhuri kwa jina la Ibn Shidad, fakihi, kadhi na mwanahistoria wa Kiislamu.

Alizaliwa mwaka 539 huko Mosul, moja ya miji ya Iraq na alihifadhi Qur'ani akiwa bado mtoto na baadaye akajifunza Hadithi, tafsiri na kusoma Qur'ani na kupata umahiri mkubwa katika taaluma hizo. Ibn Shidad alifanya safari katika nchi mbalimbali za Kiislamu kwa ajili ya kutafuta elimu.

Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni al Nawadirul Sultwaniyya, Dalailul Ah-kam na al A'swaa kinachozungumzia maisha ya Nabii Musa A.S na mapambano yake dhidi ya Firauni.   ****

Miaka 441 iliyopita katika siku kama hii ya leo alizaliwa Mulla Muhsin Faidh Kashani, aliyekuwa faqihi, mpokezi wa Hadithi, mwanafalsafa na arifu mkubwa wa Kiislamu nchini Iran.

Faidh Kashani alipata elimu za fiqhi, Hadithi, tafsiri na falsafa kwa wanazuoni wakubwa wa zama zake kama Muhammad Taqi Majlisi, Sheikh Bahai na Mulla Sadra.

Msomi huyo mkubwa ameandika vitabu vingi, mashuhuri zaidi vikiwa ni tafsiri ya Qur'ani ya al Swafi, Mafatiihu Sharaai', al Wafi na al Mahajjatul Baidhaa.    ****

Katika siku kama ya leo miaka 143 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 29 Julai 1883, alizaliwa Benito Mussolini mwanasiasa,  dikteta na mwasisi wa chama cha Kifashisti nchini Italia.

Ufashisti ni utawala wa kidikteta uliojikita katika kueneza aidiolojia ya kibaguzi na kiutaifa, kuwakandamiza wapinzani na kupotosha itikadi na fikra za wananchi. Mwaka 1922 Mussolini alinyakua wadhifa wa uwaziri mkuu wa Italia, na hivyo udikteta kuendelea kutawala nchini humo.

Muda mfupi baadaye Mussolini alishirikiana na Adolph Hitler na kuandaa mazingira ya kuanza Vita vya Pili vya Dunia.  ***

Siku kama ya leo miaka 69 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 29 Julai 1957, Umoja wa Mataifa ulianzisha Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA).

Lengo la kuanzishwa taasisi hiyo ya kimataifa, ni kusimamia shughuli zote za mitambo ya nyuklia na kuhakikisha kwamba miradi ya nyuklia duniani inatekelezwa kwa njia za amani na kutotumika kwa malengo ya kijeshi na  utengenezaji wa silaha za mauaji ya halaiki.   ***   

Siku kama ya leo miaka 45 iliyopita Abul Hassan Bani Sadr, rais aliyeuzuliwa wa Iran alikimbia nchi akiwa pamoja na kiongozi wa kundi la Munafiqin la MKO, Mas'ud Rajavi.

Siku 37 kabla yake Bani Sadr alikuwa ameuzuliwa cheo cha rais kutokana na kukosa ustahiki, kuzusha machafuko nchini na kushindwa kulinda nchi mbele ya hujuma za utawala wa Saddam Hussein.

Bani Sadr alikuwa na matumaini kwamba, mauaji ya kinyama yaliyokuwa yakifanywa na kundi la MKO yangeweza kumrejesha tena madarakani.

Hata hivyo kuchaguliwa Muhammad Rajai kuwa Rais mpya wa Jamhuri ya Kiislamu kulimvunja moyo Bani Sadr ambaye aliamua kukimbilia Ufaransa akiwa amevaa nguo za kike.   ***