Amnesty International: India inashiriki katika mauaji ya kimbari ya Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/world-i140296-amnesty_international_india_inashiriki_katika_mauaji_ya_kimbari_ya_gaza
Katika ripoti mpya iliyotolewa jana, Julai 30, Amnesty International imefichua data za forodha kuhusu usafirishaji kutoka India kuelekea Israel, ikisema kwamba New Delhi imeendelea kusafirisha vipuri vya zana za kijeshi, risasi na vifaa kwa makampuni ya Israel licha ya hatari iliyo wazi ya silaha hizo kutumika katika mauaji ya kimbari yanayoendelea huko Gaza.
(last modified 2026-07-31T03:27:24+00:00 )
Jul 31, 2026 03:20 UTC
  • Amnesty International: India inashiriki katika mauaji ya kimbari ya Gaza

Katika ripoti mpya iliyotolewa jana, Julai 30, Amnesty International imefichua data za forodha kuhusu usafirishaji kutoka India kuelekea Israel, ikisema kwamba New Delhi imeendelea kusafirisha vipuri vya zana za kijeshi, risasi na vifaa kwa makampuni ya Israel licha ya hatari iliyo wazi ya silaha hizo kutumika katika mauaji ya kimbari yanayoendelea huko Gaza.

Ripoti hiyo, yenye kichwa cha habari "Imetengenezwa India: Kutoa Silaha na Risasi kwa Israel," inaonyesha kwamba tangu Oktoba 7, 2023, karibu shehena 2,596, ikiwa ni pamoja na vipuri vya silaha ndogo, mada zxa milipuko kama vichwa vya ndege zisizo na rubani na maroketi ya mizinga, pamoja na vipuri vya magari ya kijeshi, vimetumwa kutoka India kwa makampuni makubwa ya Israel ambayo hutoa huduma za moja kwa moja kwa jeshi la utawala huo.

"Utafiti wetu unaonyesha himaya inayoendelea ya India kwa sekta ya kijeshi na ulinzi ya Israel licha ya mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa na utaala huo huko Gaza, ambayo yamekuwa yakitangazwa kote duniani karibu kila siku kwa miaka mingi," amesema Agnes Callamard, Katibu Mkuu wa Amnesty International.

Ameongeza kuwa: "Kwa kuzingatia amri za muda za Mahakama ya Kimataifa ya Haki ambazo ziliweka wazi hatari ya uwezekano wa mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina huko Gaza, maafisa wa serikali ya India hawawezi kudai kwamba hawakujua kwamba kuendelea kutoa leseni na kuwezesha usafirishaji wa silaha kwenda Israel kunaandamana na hatari kubwa ya kushiriki katika ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa."

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, makampuni yanayomilikiwa na serikali ya New Delhi ya Munitions India, Advanced Weapons and Equipment India, na India Optel ni miongoni mwa wazalishaji ambao bidhaa zao ziliingia katika mnyororo wa ugavi wa kijeshi wa Israel katika kipindi kilichochunguzwa. Makampuni haya yanamilikiwa kikamilifu na serikali ya India na yaliundwa baada ya marekebisho ya Bodi ya Viwanda vya Ordnance ya nchi hiyo mnamo 2021.

Ripoti ya Amnesty International inasema, India na Israel zimekuwa na uhusiano wa kina wa kijeshi na kiusalama kwa miongo kadhaa.

India na Tel Aviv pia zilitia saini mkataba wa makubaliano kuhusu ushirikiano wa kijeshi mwaka 2025, ukilenga kuimarisha uhusiano wa kijeshi, viwanda na kiteknolojia.

Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi pia amemtaja mwenzake wa Israel, Benjamin Netanyahu mara kwa mara kuwa ni "rafiki mpendwa," licha ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kutoa hati ya kukamatwa waziri mkuu wa Israel mwishoni mwa mwaka 2024 kwa makosa ya uhalifu wa kivita uliofanywa katika vita vya mauaji ya kimbari ya Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.