WFP yapunguza mgao wa chakula katika oparesheni zake nchini Burundi
Ongezeko kubwa la wakimbizi wanaohitaji msaada limesababisha mashinikizo makubwa kwa oparesheni ya usambazaji misaada ya chakula ya Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP).
Tangu Januari mwaka huu karibu watu 70,000, hasa wanawake, watoto na wazee, wamekimbilia Burundi wakihepa mapigano nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC ); aghaabu ya raia hao wakivuka mito hatari na kutembea umbali mrefu kutafuta usalama.
Mpango wa Chakula Duniani (WFP) umeeleza kuwa, idadi zaidi ya wakimbizi inaendelea kuwasili Burundi kila siku. Dragica Pajevic, Naibu Mkurugenzi wa WFP katika Ukanda wa Mashariki mwa Afrika ameeleza kuwa wakimbizi wanaovuka mpaka na kukimbilia katika nchi jirani na Kongo zikiwemo Rwanda, Uganda na Tanzania pia wanazidi kuongezeka kutokana na kuendelea mzozo mashariki mwa Kongo; jambo linatishia kuzidisha ukosefu wa chakula katika eneo hilo la Maziwa Makuu.
Itakumbukwa kuwa Naibu mkurugenzi wa WFP hivi sasa yupo nchini Burundi kusaidia oparesheni za kibinadamu za shirika hilo.
Wakimbizi 60,000 wamesajiliwa kupatiwa misaada ya chakula kati ya watu 70,000 waliowasili Burundi wakitokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika wiki za karibuni. Amesema shirika hilo sasa linalazimika kurekebisha ratiba zao ili kuwafikia watu wengi zaidi.
WFP inatoa misaada ya chakula kilichopikwa kwa wakimbizi wa Kongo ambao wamepatiwa makazi katika kambi za muda, mashuleni, katika viwanja vya mpira n.k.