Wakenya zaidi ya 1,000 wanashiriki katika vita vya Russia na Ukraine
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i136806-wakenya_zaidi_ya_1_000_wanashiriki_katika_vita_vya_russia_na_ukraine
Zaidi ya Wakenya 1,000 wamekwenda kupigana upande wa jeshi la Russia nchini Ukraine. Ripoti ya kijasusi iliyowasilishwa katika bunge la Kenya, imesema kuwa, wengi wa raia hao walidanganywa ili kusaini mikataba ya kijeshi.
(last modified 2026-02-19T11:56:58+00:00 )
Feb 19, 2026 11:56 UTC
  • Wakenya zaidi ya 1,000 wanashiriki katika vita vya Russia na Ukraine
    Wakenya zaidi ya 1,000 wanashiriki katika vita vya Russia na Ukraine

Zaidi ya Wakenya 1,000 wamekwenda kupigana upande wa jeshi la Russia nchini Ukraine. Ripoti ya kijasusi iliyowasilishwa katika bunge la Kenya, imesema kuwa, wengi wa raia hao walidanganywa ili kusaini mikataba ya kijeshi.

Uchunguzi mwingi wa vyombo vya habari, ukiwemo ule uliochapishwa mapema mwezi huu na AFP, umefichua jinsi Russia ilivyowashawishi wanaume kutoka nchi za Afrika kwa ahadi za ajira zenye mishahara minono, na badala yake kuwalazimisha kupigana mstari wa mbele vitani nchini Ukraine.

Uchunguzi wa pamoja uliofanywa na Idara ya Kitaifa ya Ujasusi ya Kenya na Kurugenzi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai, uliowasilishwa bungeni Jumanne, ulisema idadi ya walioajiriwa kutoka nchini humo ni "zaidi ya 1,000" -- ikiwa ni juu zaidi kuliko idadi ya "karibu watu 200" iliyotolewa na mamlaka mwezi Desemba. Kiongozi wa serikali bungeni Kimani Ichung'wah amesema Wakenya huondoka nchini kwa kutumia viza ya watalii ili kujiunga na jeshi la Russia kupitia Instanbul, Uturuki, pamoja na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Ushahidi unaonyesha kuwa, wengi kati ya walioomba kazi hiyo walikuwa maafisa wa zamani wa polisi na wanajeshi wastaafu, waliowasilisha waziwazi sifa zao za mafunzo ya kijeshi na kusema walikuwa tayari kupigana, wakitaka kazi ya kijeshi nje ya nchi.

Matokeo ya uchunguzi huo yanakadhibisha simulizi kwamba Wakenya waliokwama katika vita vya Ukraine hujikuta kwenye vita hivyo baada ya kudanganywa na maajenti.

Ushahidi unaonyesha kuwepo kwa njia iliyopangwa ya uajiri, ambapo mafunzo ya awali ya kiusalama hutolewa kama sifa ya kuajiriwa.