Nigeria: US inazilazimisha nchi za Afrika ziwapokee wakimbizi Wavenezuela
(last modified Fri, 11 Jul 2025 16:41:23 GMT )
Jul 11, 2025 16:41 UTC
  • Nigeria: US inazilazimisha nchi za Afrika ziwapokee wakimbizi Wavenezuela

Nigeria imefichua kuwa Marekani inazishinikiza nchi za bara Afrika kuwakubali wakimbizi wa Venezuela wanaofukuzwa nchini Marekani.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Nigeria amesema Marekani inazishinikiza nchi za Kiafrika kuwakubali watu waliofukuzwa Venezuela, baadhi yao kutoka gerezani moja kwa moja, lakini anasisitiza kuwa nchi hiyo yenye watu wengi zaidi barani Afrika haiwezi kuwapokea wahamiaji hao kutokana na matatizo yake yenyewe.

Utawala wa Rais Donald Trump wiki hii uliwataka marais watano wa Kiafrika kuwapokea wahamiaji kutoka nchi nyingine wakati wanapofukuzwa Marekani, maafisa wawili wanaofahamu majadiliano hayo waliambia Reuters.

Yusuf Tuggar, Waziri wa Mambo ya Nje wa Nigeria aliziambia kanali za televisheni za ndani ya nchi hiyo siku ya Alkhamisi kuwa, nchi hiyo ya Afrika Magharibi haiwezi kuafiki jambo hilo.

"Unapaswa pia kukumbuka kwamba, Marekani inazidisha mashinikizo makubwa kwa nchi za Kiafrika kukubali Wavenezuela wanaofurushwa kutoka Marekani, wengine kutoka gerezani moja kwa moja," alisema akiwa Brazil ambako alienda kushiriki mkutano wa BRICS.

"Itakuwa vigumu kwa nchi kama Nigeria kuwapokea wafungwa wa Venezuela nchini Nigeria. Tuna matatizo yetu ya kutosha," akibainisha taifa lake lenye jamii kubwa ya watu milioni 230.

Wiki hii, Trump alikuwa mwenyeji wa marais wa Liberia, Senegal, Guinea-Bissau, Mauritania na Gabon katika Ikulu ya White House. Kwa mujibu wa afisa wa Marekani na Liberia, Trump aliwasilisha mpango wa nchi za Afrika kuwapokea wahamiaji kutoka nchi nyingine wanapofukuzwa kutoka Marekani.