Mauaji ya Sayyid Hassan Nasrullah yamekuwa na taathira hasi ya kinyume cha matarajio kwa adui
Oct 04, 2024 09:44 UTC
Mwakilishi wa Harakati ya Hizbullah katika Bunge la Lebanon amesema, kuuawa shahidi Sayyid Hassan Nasrullah kumeutia moyo na kuupa ari kubwa Mhimili wa Muqawama na kuwa na taathira hasi na kinyume na iliyotarajiwa kwa utawala wa Kizayuni wa Israel.
Hassan Fadhlullah, mbunge wa Lebanon kwa tiketi ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya nchi hiyo ya Hizbullah amebainisha kuwa, msimamo ulioamuliwa kuchukuliwa na Muqawama baada ya kuuawa shahidi Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon ni kuendelea kusimama imara, kukabiliana na adui na kumzuia kufikia malengo yake.
Fadhlullah ameongeza kuwa: mauaji ya Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon, yamekuwa na taathira tofauti kwa adui kutokana kuwatia moyo wapiganaji wa Muqawama; na kwamba utawala wa Kizayuni hivi sasa unatapatapa kwenye mipaka na kumfanya Netanyahu alazimike kupanga upya mahesabu yake.

Mwakilishi wa Hizbullah katika bunge la Lebanon amebainisha: "hatuna chaguo jengine isipokuwa kusimama imara na kuilinda ardhi ya Lebanon' na akaongezea kwa kusema: "serikali ya Lebanon ina jukumu la kufanya mashauriano na mazungumzo na wala haihitaji idhini ya mtu yeyote".
Tangu Septemba 23, jeshi la la utawala wa Kizayuni wa Israel limeanzisha mashambulizi makubwa katika maeneo mbalimbali ya kusini mwa Lebanon ambayo yangali yanaendelea hadi sasa.
Wiki mbili zilizopita, utawala huo mfanya mauaji ya kimbari ulitenda jinai ya kinyama kwa kuripua vifaa vya mawasiliano vya 'Pager' vinavyotumiwa na maelfu ya Walebanoni wakiwemo wanamapambano Harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo na kuua makumi ya watu na kujeruhi zaidi ya watu elfu tatu.
Septemba 27, utawala wa kigaidi wa Israel ulimuua shahidi Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon Sayyidd Hassan Nasrullah katika shambulio la kinyama lililolenga eneo la Adh-Dhaahiya Kusini, lililoko kwenye viunga vya mji mkuu wa nchi hiyo, Beirut.../