Netanyahu: Israel haitaondoka katika maeneo ya kusini ya Syria iliyoyavamia
Waziri Mkuu wa utawala wa kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu amesema, jeshi la utawala huo halitaondoka katika maeneo liliyoyavamia na kuyakalia kwa mabavu ya kusini mwa Syria.
Akihutubia mkutano uliohudhuriwa na mabalozi wa Israel, wakuu wa misheni na maafisa wa wizara ya mambo ya nje, Netanyahu amesisitiza kwamba utawala huo wa kizayuni hautayaachia maeneo yaliyovamiwa na kukaliwa baada ya kuanguka utawala wa Bashar al-Assad mnamo Desemba 8, 2024.
"Tunataka kuhifadhi mali hizi," ametamka waziri mkuu huyo wa utawala ghasibu wa Israel, akimaanisha eneo la Jabal al-Sheikh (Mlima Hermon) na eneo la ulinzi karibu na Miinuko ya Golan inayokaliwa pia kwa mabavu na Israel tangu mwaka 1967.
Netanyahu ameongeza kuwa Israel inatarajia kufikia makubaliano na serikali ya Damascus kuhusu kuliweka eneo la kusini mwa Syria bila ya silaha wala zana zozote za kijeshi.
Waziri mkuu wa utawala wa kizayuni ametoa kauli hiyo katika hali ambayo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria, Asaad al-Shaibani alitangaza hapo awali kwamba hakutakuwa na makubaliano yoyote na Israel hadi pale itakapoondoa majeshi yake katika maeneo ya ardhi ya nchi hiyo yanayokaliwa kwa mabavu.
Hivi karibuni, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio lililosisitiza kuwa, kuendelea Israel kuikalia kwa mabavu na kuiunganisha na upande wake Miinuko ya Golan ya Syria ni "kinyume cha sheria" na likautaka utawala huo uondoke kikamilifu katika eneo hilo hadi kwenye mstari wa mpaka wa Juni 4, 1967.../