Katibu Mkuu wa Hizbullah: Lebanon inakabiliwa na uchokozi hatari wa Israel
-
Sheikh Naim Qassem
Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon Sheikh Naim Qassem amesema kuwa Lebanon inakabiliwa na uchokozi hatari na wa kujitanua wa Israel ambao unapasa kukabiliwa kwa njia zote.
Katibu Mkuu wa Hizbullah alisema hayo jana katika hotuba aliyoitoa kwa njia ya televisheni katika shughuli ya kuwaenzi wasomi waliouawa shahidi.
Sheikh Qassim amesisitiza kuwa hatua za Israel ni za kujitanua na kwamba utawala huo ghasibu hauheshimu makubaliano ya kusitisha vita yaliyofikiwa mwaka jana ingawa Lebanon na makundi yake ya Muqawama yanaheshimu makubaliano hayo.
Ameongeza kuwa, hatua za kujitanua za utawala wa Kizayuni si kwa ajili ya kuupokonya silaha Muqawama bali kuikalia kwa mabavu Lebanon na kuanza kutekeleza kile kinachojulikana kama "Israel Kubwa."
Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesisitiza kuwa Marekani na Israel hazipasi kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo, au mikakati yake ya ulinzi.
Amesema, silaha za Muqawama na uwezo wa kiulinzi wa Lebanon wa kukabiliana na uchokozo wowote si suala la kujadiliwa.
"Tutajihami sisi wenyewe, watu wetu na nchi yetu na tuko tayari kujitolea, hatutasalimu amri," amesema Sheikh Naim Qassim.
Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon ameitaka serikali ya nchi hiyo kutimiza majukumu yake hususan katika kulinda mamlaka ya kujitawala, kuijenga nchi na kuimarisha uchumi na kuongeza kuwa, madola ya kibeberu yanafanya kila liwezekanalo kuifuta Hizbollah kwa sababu ya mradi wake wa kitaifa, ambao unatoa wito wa ukombozi, uhuru na utu.